Pengine hii yaweza kuwa ni
historia; kuanzia Machi 7 walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaofundisha
shule za Serikali za msingi na sekondari, hawatalipa nauli kwenye kwenye
daladala wakati wakienda na kutoka kazini.
Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alitangaza hayo jana mbele ya viongozi
wa vyama vya usafirishaji abiria na madereva Mkoa wa Dar es Salaam.
Makonda
alisema wazo lake la kutaka walimu wasafiri bure limeungwa mkono na
viongozi wa vyama vya wasafirishaji abiria na wamiliki wa daladala na
kwamba kilichobaki ni kuanza kutoa huduma hiyo.
“Awali,
wazo langu ilikuwa walimu wa Wilaya ya Kinondoni ninayoiongoza, ndiyo
wafanyiwe utaratibu wa kusafiri bure lakini wadau wa usafirishaji
wakashauri iwe kwa mkoa mzima. Nikamweleza mkuu wa mkoa na akaniruhusu
tufanye hivyo mkoa mzima,” alisema Makonda ambaye mpango wake wa
kuchangia ujenzi wa shule umemhakikishia cheo baada ya Rais John
Magufuli kuguswa.
Makonda alisema kuanzia leo, wakuu wa shule za msingi watakakiwa kuwatengenezea walimu wao vitambulisho kwa ajili ya usafiri.
Mambo manne
Alisema
vitambulisho hivyo ambavyo vitavaliwa wakati wa kupanda daladala,
vitatakiwa kuwa na picha ya mwalimu, jina lake kamili na jina la shule
anayofundisha.
Mkuu wa wilaya hiyo alisema vitu vingine
vinavyotakiwa kuwa kwenye vitambulisho hivyo ni saini ya Makonda ili
kuepuka udanganyifu na namba ya simu ya mkuu wa shule husika.
Alisema
baada ya vitambulisho kukamilika, walimu watapanda bure katika daladala
lolote wakati wa kwenda kazini kuanzia saa 11.30 hadi saa 2.00 asubuhi
na kwamba wakati wanarejea nyumbani huduma hiyo itaanza saa 9.00 alasiri
hadi saa 11.00 jioni.
Makonda alisema huduma hiyo ya
usafiri bure kwa walimu itatolewa siku tano kwa wiki kuanzia Jumatatu
hadi Ijumaa na kwamba siku za Jumamosi, Jumapili na sikukuu watatakiwa
kulipia.
“Huo ni muda ambao wamiliki wamekubali
kusafirisha walimu bure kwenda kazini na kurudi nyumbani. Nje ya muda
huo walimu watatakiwa kulipa nauli kama kawaida,” alisema.
Makonda
alisema baada ya Rais Magufuli kutangaza elimu bure, aliona amuunge
mkono kwa kuweka mazingira yatakayorahisisha utendaji kazi wa walimu.
Mwenyekiti
wa Chama cha Wamiliki wa Daladala cha Dar es Salaam (Darcoba), Sabri
Mabruki alisema wamekubali kutoa usafiri bure kwa walimu ili kumuunga
mkono Magufuli katika juhudi zake za kuboresha elimu. “Tumeletewa ombi
na mkuu wa wilaya akitueleza kuhusu wazo la kutaka kusafirisha walimu
bure. Kwa namna Makonda na Rais wanavyofanya kazi, hatukuwa na kinyongo
zaidi ya kukubali ombi hilo,” alisema.
Akiunga mkono
huduma hiyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wasafirishaji Abiria (Uwadar),
William Masanja alisema elimu bure haiwezi kufanikiwa kama mazingira ya
kazi ya walimu yatakuwa magumu.
“Ndiyo maana
tulivyoambiwa na mkuu wetu wa wilaya, hatukuwa na muda wa kupoteza zaidi
ya kukubali ombi lake. Tumejipanga kuwasafirisha walimu ili waweze
kufundisha watoto wetu,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama
Wafanyakazi Madereva Tanzania (Tadwu), Shaaban Mdemu aliwataka walimu
kuzingatia muda uliopangwa kusafiri bure ili kuondoa usumbufu.
Aliwataka
wamiliki wa daladala kuwa wasikivu iwapo wataambiwa na madereva wao
kuwa mapato ya siku yamepungua kutokana na kuwepo kwa huduma hiyo.
Akizungumzia
uamuzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT),
Ezekiah Oluoch alisema jambo hilo likitekelezeka, Makonda atakuwa
kiongozi wa mfano hapa nchini kuthamini kazi za walimu.
“Mpango huu unatakiwa kupongezwa, kuungwa mkono na wadau wa elimu. Tunahitaji kuwapa moyo viongozi wabunifu kama hawa,” alisema.
Alisema walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam wanatumia wastani wa Sh3,000 kwa siku kwa ajili ya usafiri wa daladala.
“Sehemu kubwa ya mishahara ya walimu inatumiwa kwa ajili ya usafiri, mpango huu utakuwa mkombozi kwao,” alisema.
Alisema kama mpango huo utafanikiwa mkoani Dar es Salaam, unatakiwa kuanzishwa kote nchini.
Hata
hivyo, Oluoch alipendekeza mpango huo utungiwe kanuni ili makubaliano
hayo yaendelee kudumu hata kama viongozi hao hawatakuwapo Dar es Salaam.