15 Jul 2016


SURA SITA ZA KITABU
Utangulizi
Haya shime piga konde, mambo sasa kuandika,
Mithili maji mbande, yanotaka kumwagika,
Natanguli….chondechonde, sura sita bila shaka
Lengo kinyume cha mwande, uwanja uje safika,
Tupambane tuyashinde, ili tuje heshimika,
Sura sita kila pande, zimenena bila shaka,

Sura ya kwanza
Yarabi nipe imani, sura hii kueleza,
Yanofanywa sakafuni , mimi yananishangaza,
Na vifo vya hadharani, albino wapoteza,
Ni dhambi iso kifani, nchi twaitelekeza,
Tupambane kwa yakini, kwa umoja tutaweza,
Tudumishe na amani, na sifa kuendeleza,
Tuzidishe ikisiri, tokomeza mauwaji.

Sura ya pili
Sura hii si sharifu, inaitwa “ugaidi”
Sura hii si nadhifu, kueleza imebidi,
Nchi wazifanya chafu, mwanadamu makusudi,
Kuua kwa israfu, duniani kumezidi,
Afrika sasa hofu, mashariki ni zaidi,
Tuwatoe waarifu, tupambane kwa jihadi,
Afrika iwe safi, iwe safi na nadhifu.

Sura ya tatu
Haya shime kwa salamu,hii sura ni makini,
Ina mambo ya muhimu, yalo bora na thamani,
Haya mambo ya kalamu, hayaitaji umbini,
Yanaitaji nidhamu, pamoja na darubini,
Kutazama kufahamu, tunapanda tupo chini,
Kwa wadau na walimu, tufanye kazi nyanjani,
Tuiboreshe elimu, vizazi visipotee.

Sura ya nne
Jama sili nikashiba, natafuta koti langu,
Koti hilo ndio tiba, visiwani bara kwangu,
Kwa famili ndio baba, binadamu moyo wangu,
nikilikosa msiba, itazikwa nchi yangu,
kubwa maoni ya huba, yatoke kwako na kwangu,
tuitetee katiba, tutetee kwa uchungu,
bila katiba ni sawa, gari bila mataili.

Sura ya tano
Sura hii ya vijana, wa rika lile shufufu,
Wavulana wasichana, wahusika maarufu,
Mitandaoni kwa sana, Kuperuzi picha chafu,
Matumizi yaso mana, kutumia bila hofu,
Kuna baadhi vijana, tumia kwa unadhifu,
Mambo mema kupashana, na kukemea machafu,
Ya jamii mitandao, tuitumie muluwa.

Sura ya sita
Kuna mapacha wawili, sasa wana jina moja,
Ukimuita wa pili, wanaitika pamoja,
Waliungana wawili, hivi sasa ni mmoja,
Wametoka huko mbali, waliungana kwa hoja,
Na mchanga wa halali, walichanganya pamoja,
Kulipinga jambo hili, ni hoja si kubwabwaja,
Tudumishe muungano, Tanzania songa mbele.

hitimisho
Hitimisho langu leo, lina mambo kadharika,
Na walio wengi wao, nahodha taka kushika,
Kutangaza nia zao, lengo chombo kupeleka,
Wananchi kazi yao, yupi safi kumuweka,
Bila kujali wa kwao, au wapi anatoka,
Kiongozi ndio ngao, ili bora imarika
Uchaguzi ukifika, weka nia piga kura

                                   AHSANTE

Maridadi mwili wangu, sifa zake pendezea,
Shukrani pewa Mungu,Aliyenitunukia,
Viganja weka uvungu, Ili peni kushikia,
Busara na zako huba, Ahsante kwa kuniumba.

Mikono ilo imara, Viganja panga vidole,
rahisi iwe kuchora, kuyaeleza ya mbele,
Jenga jamii imara, Kama mwalimu wa shule,
Busara na zako huba, Ahsante kwa kuniumba.

Ukapachika miguu, Niweze kutembelea,
Nipite chini na juu, Siri nyeti fuatia,
Nikizipata walau, Mkono kuandikia,
Busara na zako huba, Ahsante kwa kuniumba.

Ukaniweka na macho,Nipate kuonelea,
Pale kwenye jingi ficho, Niweze kulifichua,
Alo nacho aso nacho, wapate kuheshimia,
Busara na zako huba, Ahsante kwa kuniumba.

Leo mimi nichochole, Ila mkwasi wa shule,
Shika peni kwa vidole, kukomboa uma ule,
Nitoe siri za mule, zilofichwa toka kale,
Busara na zako huba, Ahsante kwa kuniumba.

Ukanipa na akili, Zipate kuniongoza,
Niepuke ufedhuli, Ili nipate mwangaza,
Maisha nisije feli, kwenye fifi rangi koza,
Busara na zako huba, Ahsante kwa kuniumba.

Ahsante kwa majukumu, Mimi saizi wa haki,
Kwa mburura mi mwalimu, Epuka fanya fasiki,
Kwa kutumia kalamu, Mzawa si mamluki,
Busara zako huba, Ahsante kwa kuniumba.

Ukaniwekea pua, niweze kupumulia,
          Vizuri vya kuvutia, vilo mbali kuhisia,
Na vingine pia pia,, ndani kunipachikia,
Busara na zako huba, Ahsante kwa kuniumba.

Ukanipa na mtutu, na rasasi zake mbili,
Niweze kututututu, pale penye stahili,
Nipate sifa ya mtu, niipate kulihali,
Busara na zako huba, Ahsante kwa kuniumba.

Ukanipa na uwezo, kipaji kweli kipaji,
Kutunga kwa michirizo, naogopa utegezi,
Mashairi si mchezo, mjuzi ndo mteguzi,
Busara na zako huba, Ahsante kwa kuniumba.

NAJUTA

Najuta kula papai ,lenye sumu ndani yake,

Papai kwenye kalai, tafuna na mbegu zake,

Lenye sumu halifai,kutafuna kwa makeke,

Najuta kula papai, utomvu wake balaa.


Mnyamavu kwangu mimi, kupenda papai bichi,

Nikajingata ulimi, leo nasema sifichi,

kilicho nidhuru mimi, papai chini chikichi,

Najuta kula papai, utomvu wake balaa.


Papai liso maganda, nilikula kwa fasiki,

utamu shuka napanda, kuachilia sitaki,

Na utovu wa maganda, kuruka kama bunduki,

Najuta kula papai, utomvu wake balaa.


Papai kumenya chini, uvimbe ukaja juu,

Nakufukuzwa shuleni, siyesiki la mkuu ,

wazazi sasa nyumbani, subiri na ujukuu,

Najuta kula papai, utomvu wake balaa.


Sasa nakosa masomo, kwa tamaa ya papai,

sasa niko na kilimo, uzembe wangu shingai,

Pia sina msimamo, wenye vyao wajidai,

Najuta kula papai, utomvu wake balaa,

 

Sasa nipo na kilimo, uzembe wangu shingai,

Pia sina msimamo, wenye vyao wajidai,

Hili kwangu kubwa somo, nilikuwa silijui,

Najuta kula papai, utomvu wake balaa,


Ila kinachoniuma, muhusika kakimbia,

Papai kwenye kisima, kaosha na kutimua,

leo kwangu ni mlima, amekimbia kulea,

Najuta kula papai, utomvu wake balaa.


Mwisho wa yangu habari, tamati nimefikia,

Kikubwa ni ushauri, mapema kuwaachia,

Maboga ndiyo mazuri, papai acha chezea.

Najuta kula papai, utomvu wake balaa


MBILI ZISIZO HALALI
Leo niwajuze kweli, walisema watu jana,
Mbili zisizo halali, kakataa sub- hana,
Leo zakaa mahali, na hofu kwao hakuna,
Mbili zisizo halali,yarabi amekataza.

Niwajuze kwelikweli, mnisikie kwa kina,
Mmepunguza makali, amri na kuikana,
Mmekaa ndani tuli,wala vibali hamna,
Mbili zisizo halali,yarabi amekataza.

Wajifanya jemidali, unatamba kila kona,
Hayo sio maadili, hapo thawabu hakuna,
Mbili zisizo halali, mungu kazikana sana,
Mbili zisizo halali,yarabi amekataza.

Binti aliyenadhifu, haishi bila nikhai,
Kufanya mambo machafu,chondechonde nawasii,
Mjifunze maradufu, mzidishe uwalii,
Mbili zisizo halali,yarabi amekataza.

Kwa wasomi wa vyuoni, na vijana wa kileo,
Kumfungia chumbani, mtoto wa mwenzio,
Wafaidi vitu ndani, utazani ni mkeo,
Mbili zisizo halali,yarabi amekataza.

Ukitaka awe ndani , muongozo ufuatao,
Cha kwanza nenda nyumbani kuona wazazi wao,
Msikiti kanisani, watoe baraka zao,
Kukabidhi kwa amani,sasa huyo ni mkeo,
Mbili zisizo halali,yarabi amekataza.

Urudi nae nyumbani, yarabi katakdiri,
Ndoa pokea mbinguni , na tena kaibashiri,
Mtaishi kwa amani, ndoa yenu kunawiri,
Mbili zisizo halali,yarabi amekataza.

Sasa mbili ni halali, na sunna mmetimiza,
Yarabi wape sahili,hekima kutekeleza,
Mjitoe kwa sabili,kufuata yake muweza,
Mbili zisizo halali,yarabi amekataza.


TUNDA LISILO NA MBEGU
Fumbo hili nalifumba, ninawafumbia nyie,
Kwa shangazi na mjomba, yenu radhi mniwie,
Nataka leo kutamba, walimwengu wanijue,
Tunda lisilo na mbegu, tunda hilo tunda gani.

Tunda hili tunda gani, linanoga hata bichi,
Sijui hata kwa nini, zaidi ya mchikichi,
Halifanani fanani, na embe na parachichi,
Tunda lisilo na mbegu, tunda hilo tunda gani.

Nilipokuwa polini, katikati ya msitu,
Inama okota chini,pasi kuniona watu,
Kuosha kumenya ndani, wala sikuona kitu,
Tunda lisilo na mbegu, tunda hilo tunda gani.

Tunda lina rangirangi, zile fifi na kukoza,
Tunda lina nyama nyingi, za kukata na kutunza,
Tunda washangaa wengi, kutafunwa lasinyanza,
Tunda lisilo na mbegu, tunda hilo tunda gani.

Likiiva lasinyaa, halina thamani tena,
Kama bichi latambaa,pata menya kutafuna,
Ila halipozi njaa,tafuna na lake shina,
Tunda lisilo na mbegu, tunda hilo tunda gani.

Na matunda anuai, duniani yanalika,
Kama epo na papai, na dhabibu kadharika,
Na mengine siyajui, wavuli nawaswalika,
Tunda lisilo na mbegu, tunda hilo tunda gani.

Twaweza kusema ndizi, ila umbo tofauti,
Au umbile la nazi, ya uwazi katikati,
Tunda hili ni azizi, ni dogo kwa wake mti,
Tunda lisilo na mbegu, tunda hilo tunda gani.

Toka enzi za mababu, tunda likipatikana,
Tunda hili la ajabu, kaliumba sub-hana,
Naomba mnipe jibu, na mifano yenye mana,
Tunda lisilo na mbegu, tunda hilo tunda gani.

Maajabu ya manani, inabidi tukubali,
Tunda leta duniani,huwezi pata manzili,
Ndugu zangu wazuoni,kaa chini mjadili,
Tunda lisilo na mbegu, tunda hilo tunda gani.

Wanagenzi mashuhuri, nanyi swali nawachia,
Bora niwape dodori, rangi yake kahawia,
Jibu likiwa tayari, msisite kuniambia,
Tunda lisilo na mbegu, tunda hilo tunda gani.
BABA AMESAHULIKA
Haya shime nijuzeni, vipi mama peke yake,
Mnijuze kwa makini, mnipe sababu zake,
Nawauliza kwa nini, baba hana shufu zake,
Mchango wake u wapi , baba amesahulika,

Waimbaji redioni, kila siku wasikike,
Na sifa zidi tisini,zote mpa mama yake,
Nampenda kama nini,mama yangu peke yake,
Mchango wake u wapi , baba amesahulika,

Tunapompa thamani,tutazame chanzo chake,
Ulipokuwa tumboni, ni nani sababu yake
Aliyempa idhini, na zile huduma zake,
Mchango wake u wapi , baba amesahulika,

Pamoja na mitiani, mama na mtoto wake,
Baba akiwa kazini,toroka ofisi yake,
Huku maziwa dumuni, letea mtoto wake,
Mchango wake u wapi , baba amesahulika,

Akisafiri nchini, simu kwanza mke wake,
Habari hapo nyumbani, cha pili mtoto wake,
Vipi anashida gani, muuliza mke wake,
Mchango wake u wapi , baba amesahulika,

Baba Beni baba Beni, mimi Beni mama yake,
Mwanetu yu taabani,jambo gani lifanyike,
Naomba uje nyumbani, tena fanya uharake,
Anatatizo tumboni, ndio chanzo cha upweke,
Mchango wake u wapi , baba amesahulika,

Baba hupita dukani,anunue dawa zake,
Anawasili nyumbani, ana hofu na mwanake,
Mama Beni mama Beni, maji moto uinjike,
Beni aoge mwilini,ameze na dawa zake,
Kesho hospitalini,apate vipimo vyake,
Mchango wake u wapi , baba amesahulika,

Nawaasa wanajemi, na baba athaminike,
Katuleta duniani, sio mama peke yake,
Msifu baba jamani, waandishi muandike,
Mchango wake u wapi , baba amesahulika,

Powered by Blogger.

Wasiliana nami papo kwa papo

Name

Email *

Message *

Ads 468x60px

Breaking News

Top Featured

Featured Posts

Sample text

Sample Text

Recomended

Facebook

Advertise

Most Popular

Connect With Us

Followers

Social Icons

Pages

Pages

BTricks

Pages

Popular posts

Tafuta chochote ukiwa hapahapa

Kategori

Recent Comments

You can replace this text by going to "Layout" and then "Page Elements" section. Edit " About "

recent posts

Video Of Day

TRANSLATE

Instructions

Video

Flickr Images

FURAHIA UWEPO WAKO HAPA

Logo Design by FlamingText.com
Logo Design by FlamingText.com

Imetembelewa mara

TAKWIMU ZA WATEMBELEAJI

Popular Posts

SAJIRI

Definition List

premium-wordpress-themes.org