MAKALA FUPI YA DONDOO YA TAALUMA YA TAFSIRI NA
UKALIMANI.
MAALUMU KWA WANAFUNZI WA KIDATO CHA 5 & 6.
SHULE YA UPILI AGAPE – MBAGALA.
IMETAYARISHWA NA :
MTILA BAHATI NA MPUNDA H. MUHIDINI
2018
Utangulizi
Kwanza,
tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwa Allah
kwa kutujalia ilhamu, siha na raghba katika mchakato mzima wa kuandika Makala
haya. Tusingefua dafu pasi na Baraka zake yeye.
Jitihada zetu za
kuandaa Makala haya ya tafsiri na ukalimani ni za kweli, zilizojaa neema na nia
ya kusaidia kusukuma gurudumu la elimu nchini Tanzania na katika jamii nzima ya
Afrika Mashariki kwa ujumla.
Dondoo hizi
chache katika Makala haya, zimehawilisha kutoka katika mswada mkuu wa kitabu
cha masuala ya tafsiri na ukalimani kinachoandaliwa na waandishi Mtila bahati
pamoja na Muhidini H. Mpunda. Kinachotarajiwa kuzinduliwa mwaka huu 2018. Pia
dondoo hizi zimezingatia sana mahitaji ya wanafunzi wa shule ya upili AGAPE-
MBAGALA baada ya kufanya mazungumzo na kuchangia mawazo kuhusu vipengele kadhaa
vinavyochanganya katika taaluma hii ya tafsiri na ukalimani, hatimaye, kuamua
kuyafanyia kazi mawazo yao ili kutatua changamoto hiyo.
Ni matumaini
yetu dondoo hizi chache zinaweza kusaidia kwa namna moja au nyingine kutatua
changamoto katika baadhi ya vipengele vichache tulivyovifanyia kazi.
Tutangulize
shukrani zetu za dhati kwa mkuu wa shule kwa kutupatia ridhaa na kutukaribisha
shuleni kwake, pili idara ya Kiswahili pamoja na walimu wengine wa shule ya
sekondari Agape kwa ushirikiano wa hali na mali, baadhi yao ni mwl Bariki
Kyando, Baraka Kalinga na Pendo Nicholous.
Mwisho,
tunaitimisha kwa kusema Makala hii tunaitabaruku kwa walimu na wanafunzi wote
wa kidato cha tano na sita kwa vizazi na vizazi watakaojiunga na shule ya upili
Agape.
Mtila bahati
Barua pepe:bamtila@gmail.com
Blog: mtilabahati.blogspot.com
Rununu: 0675 975 756/0683 797 770
Dar- es- salaam
Mpunda H. Muhidini
Barua pepe: muhidinimpunda@gmail.com
Rununu: 0656 984 873/0692 468 788
Dar- es- salaam
TAFSIRI
Maana ya Tafsiri
Tafsiri ni
taaluma inayojihusisha na uhawilishaji wa mawazo au ujumbe ulio katika
maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa kusudi maalum.
Dhana za msingi katika tafsiri
Fasili ni kufafanua maana ya neno kwa kina.
Kurudufu ni kunakili alama au kitu kama kilivyo.
Kwa hiyo, urudufu unaweza kuitwa ni unakili. Kwa mujibu wa TUKI (2013),
kunakili ni kufuatisha au kutoa kivuli cha mchoro au maandishi kama yalivyo.
Ukafsiri ni mchakato wa kitendo cha kukafsiri.
Kukafsiri ni kuhawilisha ujumbe kutoka matini andishi kwenda mazungumzo au
kutoka mazungumzo kwenda katika maandishi kutoka lugha chasili hadi lugha lengwa,
kwa kuzingatia muktadha, isimu na utamaduni wa lugha zinazohusika.Mfano mzuri
ni sinema ambazo wahusika wake wanakuwa wanaongea lakini maneno yake
yanaandikwa katika runinga chini.
Matini ni kifungu cha maneno kilichoandikwa
ambacho kimebeba maana au ujumbe fulani.
Matini chanzi ni matini inayotafsiriwa kwenda lugha nyingine
Matini lengwa ni matini iliyotafsiriwa katika
lugha lengwa.
Lugha chanzi ni lugha iliyotumiwa katika mchakato wa
kuandaa matini chanzi
Lugha lengwa ni lugha inayotumiwa katika mchakato wa
kuunda matini lengwa.
Mfasiri mtu mwenye taaluma au tajiriba ya
kutafsiri na ambaye amejikita katika shughuli hizo. Pia lazima awe mjuzi wa
lugha zisizopungua mbili.
Nduni za mfasiri kabambe au jamali
Zifuatazo ni
baadhi ya sifa au nduni za mfasiri jamali;
(i)
Awe
mwenye taaluma na ujuzi wa tafsiri mfano awe amesomea kozi ya taaluma ya
tafsiri au amepitia mafunzo fulani,
(ii)
Awe
na utashi wa kuibua hisia sawa kwa wapokezi wa ujumbe.
(iii)
Awe
na tajiriba katika taaluma zingine mfano isimu jamii na isimu ethnolojia.
(iv)
Awe
mzawa au mbobevu wa tamaduni mbalimbali.Mwenye kipaji au taaluma ya uhariri,
uandishi, na uhakiki wa matini mbalimbali.
(v)
Awe na stadi za uhakiki matini.
(vi)
Awe
na maarifa au ujuzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano yaani (TEHAMA)
(vii)
Awe
na tajiriba kubwa ya usomaji wa aina mbalimbali za tafsiri.
(viii)
Awe
na tabia yakushirikiana na watu wengine katika shughuli za kufasiri.
DHIMA ZA TAFSIRI
Tafsiri ina
majukumu lukuki ndani ya jamii hususani katika ulimwengu wa sasa wa sayansi na
technolojia. Baadhi ya dhima za tafsiri ni kama ifuatavyo :-
(i)
Kueneza
utamaduni wa jamii ya lugha chasili, kupitia kutafsiri kazi mbalimbali za
kitaaluma pamoja na za kifasihi imesaidia kujua asili ya utamaduni wa lugha
chasili. Mfano tamthilia ya “nitaoa nikipenda” imetungwa katika mazingira ya
jamii ya kikuyu na kwa mara ya kwanza iliandikwa kwa lugha hiyohiyo lakini
baada ya kutafsiriwa kwa kingereza (I will marry when I want) wasomaji wengi
waliweza kujua mila na desturi za jamii ya wakikuyu.
(ii)
Kutambua
historia ya jamii husika, kazi nyingi sana za kale zilikuwa zimeandikwa
katika lugha ya eneo fulani mahususi.
Mfano tamthilia ya Sofokile iitwayo
“ Mfalme edipode” iliandikwa kwa
kigiriki kama lugha chasili ilifanikiwa kufanyanyiwa tafsiri kwa kiingereza na
hatimaye katika lugha ya Kiswahili.
(iii)
Tafsiri husaidia
kujua itikadi ya jamii husika,
Itikadi ni imani kuhusu jambo fulani,waandishi
wengi hupenda kuandika kazi zao huku
wakitanguliza itikadi mbele. Tafsiri inapochukua mkondo wake ndipo tunakuja
kujua kumbe mwandishi fulani ana itikadi gani au jamii Fulani ina itikadi gani.
(iv)
Tafsiri kama mbinu
ya mawasiliano.
Tafsii hutumika kutolea maelekezo ya biashara kama vile maelekezo ya jinsi ya
kutumia bidhaa zinazouzwa na kusafirishwa kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine
sanjali na matangazo ya kitalii. Pia, tafsiri hutumika katika vyombo vya
habari na katika vitabu vya kufundishia
na kujifunzia.
(v)
Tafsiri kama
soko la ajira,
wataalamu wengi wa tafsiri wanafanya kazi mbalimbali kama sehemu ya kipato na
ofisi kwa ujumla watu hufanya tafsiri katika kazi mbalimbali mfano mikataba ya
kimataifa, nyaraka za kiserikali ( sheria mbalimbali pamoja na katiba) na
mashirika binafsi, pia tafsiri ya vitabu mbalimbali husaidia waandishi kupata
kipato binafsi.
(vi)
Tafsiri kama
mbinu ya kujifunza lugha. Tafsiri hapa husaidia kukuza lugha lengwa mfano
fasihi ya lugha lengwa hunufaika kwa kuingizwa kwa vipengele kadhaa vya lugha
hususani misemo na methali ambazo hazikuwepo katika lugha hiyo lengwa.
(vii)
Tafsiri hutumika
katika nyanja ya elimu, sayansi na teknolojia, hapa tunaangalia maendeleo
ya sayansi na technolojia ya nchi za Ulaya yametokana na maarifa yaliyoibiwa
kutoka katika nchi za kiarabu mfano Misri. Watu wa Ulaya walifanikiwa kutafsiri
vitabu na kujifunza maarifa na ujuzi wa watu wa Misri hatimaye nchi za Ulaya
ziliendelea kupiga hatua. Pia nchini Tanzania mfumo wa elimumsingi unatumia
lugha ya Kiswahili hivyo wataalam walilazimika kutafsiri vitabu kwa lugha ya Kiwahili
ili viendane na lugha yao.
(viii)
Kueneza na
kuongeza wasomaji wa fasihi andishi, katika kila kona ya dunia kuna
waandishi wa kazi za fasihi kutokana na watu wengi kutofahamu lugha nyingi
husababisha watu kukosa maarifa mapya ya waandishi wengine, hivyo basi taaluma
ya tafsiri imesaidia sana watu wa mataifa mbalimbali kusoma kazi moja ikiwa
katika lugha mbalimbali mfano tamthilia, ya mfalme edipode imetafsiriwa katika
Kiswahili kutoka Kiingereza wakati asili ya kazi hii ni Kigiriki.
(ix)
Tafsiri kama
kiliwazo cha nafsi ya mfasiri. Humfanya mfasiri kuutuliza mtima wake
kadri anavyofanikiwa kutatua matatizo yake ya kifasiri. Utafutaji wa visawe
katika lugha lengwa si kazi rahisi hivyo basi mfasiri anapopata visawe hivyo
kutoka katika vyanzo mbalimbali
hufarijika kwa kupata mafanikio makubwa sana.
(x)
Tafsiri
imesaidia kuendeleza dini.Malenya (2016) dini ni imani ya mtu juu ya kitu
fulani. Hapa tunaona maandiko mbalimbali yanayohusu masuala ya kidini
yamefanyiwa tafsiri katika lugha mbalimbali mfano Biblia Takatifu iliandikwa
katika lugha ya Kiebrania ikaambaa amba katika lugha mbalimbali mpaka kwenye
kiingereza na hatimaye kwenye kiswahili na hadi kwenye lugha za makabila. Pia
Qur- an Tukufu iliyoshushwa katika lugha ya kiarabu lakini mpaka hivi sasa kuna
tafsiri nyingi katika lugha mbalimbali mfano Kiswahili na Kiingereza na Kijaluo.
Mfano Profesa Omar Al Bashiri ametafsiri Qur- an tukufu kwenda Kijaluo
Mbinu au njia za Tafsiri
kielelezo
kifuatacho kinafafanua njia zinazotumia kufanya tafsiri
MBINU ZA TAFSIRI
(i) Tafsiri
ya neno kwa neno
Hii ni aina ya
tafsiri ambayo mofimu (mofu) na maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke kwa
kuzingatia maana zake za msingi bila kujali muktadha. Mdee, (1986:87) anasema,
“Wafasiri aghalabu tafsiri zao huhitaji neno kwa neno katika dhana fulani
badala ya maelezo.” Katika aina hii ya
tafsiri mpangilio wa mofimu na maneno ya lugha chanzi hubakia vilevile bila
kubadilika..mifano,
Mfano 1.
Kiswahili: Alilala hadi asubuhi.
Kingereza: He/past/sleep/until/morning.
Mfano 2.
Kiswahili: Alikimbia mpaka ofisini kwake
Kingereza: He/past/run/until/office/his.
Mfano 3.
Kimakuwa:mustadi anolya ishima
Kingereza: mustadi/present/ eat/ugali.
Ubora wa mbinu hii
§ humsaidia mtu
kuelewa muundo wa lugha chanzi na jinsi lugha chanzi inavyofanya kazi.
§ Husaidia kuelewa
utofauti wa mpangilio wa maumbo katika sentensi za lugha tofauti.
Udhaifu wa mbinu hii
§ Upungufu mkubwa wa njia hii ni kuwa, huwa haitoi maana
lengwa kwa uwazi zaidi.
(ii)Tafsiri
sisisi
Hii ni aina ya
tafsiri ambayo maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke kwa kuzingatia maana za
msingi katika lugha chanzi bila kujali sana muktadha lakini ni tafsiri
inayofuata mfumo wa kisarufi hasa kipengele cha kisintaksia ya lugha lengwa.
Ebu tuangalie mifano ifuatayo:
Kingereza: He was taken at the Central bus Station
(bus)
Kiswahili: Alipelekwa kwenye kituo cha kati cha
mabasi.
Badala ya kuwa: Alipelekwa stendi kuu ya mabasi.
Ubora wa mbinu hii
ü Husaidia
kufasiri dhana zisizofasirika kirahisi kama vile misemo, nahau, majina ya
khanga n.k.
ü Ni mbinu bora
ukilinganisha na tafsiri ya neno kwa neno.
Udhaifu wa mbinu hii
ü Si nzuri
kutumika katika matini ndefu
(iii)Tafsiri
ya kisemantiki
Hii ni aina ya
tafsiri ambayo mfasiri huegemea zaidi kwenye lugha chanzi. Katika aina hii ya
tafsiri, mfasiri hufasiri kila neno katika sentensi jinsi lilivyo lakini kwa
kufuata sarufi hususani vipengele vya kisemantiki na kisintaksia ya lugha
chanzi. Inaitwa tafsiri ya kisemantiki kwa sababu, mfasiri anapofasiri hutakiwa
kuweka mkazo kwenye maana ya matini kama ilivyokusudiwa na mwandishi wa matini
chanzi.
Katika aina hii
ya tafsiri, masahihisho au urekebishaji wa neno au jambo lolote unalodhani
limekosewa hairuhusiwi isipokuwa unaweza kuweka hayo marekebisho au ufafanuzi
katika tanbihi. Sasa tuanglialie baadhi ya mifano ya aina hii ya tafsiri:
Kiswahili: Alikwenda mpaka hospitali
Kingereza:
He went up to hospitali
Kingereza:
Aisha married salumu
Kiswahili:
Aisha alimwoa salumu
Faida ya mbinu hii
ü Mbinu hii
huingiza miundo ya misemo kutoka lugha chanzi. Mfano lugha ya Kiswahili
imepokea miundo mipya ya misemo kutoka lugha ya Kingereza, baadhi ya miundo
hiyo ni kama vile all ni all - yote
kwa yote, at the end of the day –
mwisho wa siku.
Udhaifu
ü Tafsiri hii ni
ya kimzunguko na ya kiufafanuzi sana.
ü Haina vionjo na
humfikirisha sana msomaji
(iv)Tafsiri
ya mawasiliano
Ni aina ya
tafsiri ambayo mfasiri ana uhuru wa kutumia visawe (maneno) yanayoweza kutoa
athari sawa na ilivyo katika matini chasili. Kikubwa katika aina hii ya tafsiri
hulenga kuhawilisha athari iliyopo katika matini chasili hadi katika matini
lengwa.
Mfano,
Kiingereza:
Tanzania National Electric Supply
Kiswahili:
Shirika la Umeme Tanzania
Kiingereza:
Wonders never end
Kiswahili: Ukistaajabu
ya Musa utayaona ya Firauni.
Kiswahili :
mwenda tezi na omo marejeo ngamani
Kiingereza: Go
east, go west, home is best
Faharasa
Baadhi ya
wataalamu wameelezea mbinu tano za tafsiri wakijumlisha tafsiri neno kwa neno,
sisisi, semantiki (maana), mawasiliano na tafsiri mkopo
Tafsiri mkopo ni
aina ya tafsiri amabyo mfasiri hutafsiri moja kwa moja mofimu za neno
lililokopwa.
UKALIMANI
Maana ya Ukalimani
Ukalimani ni taaluma inayojihusisha na uhamishaji
wa ujumbe fasaha ulio katika mazungumzo ya mdomo kutoka lugha chasili kwenda
lugha lengwa.
Mkalimani ni mtu yoyote mwenye taaluma na tajiriba
ya ukalimani na anayejihusisha na kukalimani.
Aina za ukalimani
Aina za
ukalimani zinaweza kuanishwa katika vigezo vikuu viwili navyo ni:-
kigezo cha Muktadha au mazingira ya utendekaji wa
tukio.
Kwa kujikita
katika kigezo hiki cha muktadha na utendekaji wa tukio tunapata aina zifuatazo
za ukalimani:-
Ukalimani wa Kijamii. Huu ni
ukalimani ambao hufanywa katika masuala mbalimbali ya kijamii kama vile afya,
ujenzi wa shule, maji, umeme na mihadhara ya kidini nk.
Ukalimani wa Mikutano na Makongamano; Huu ni
ukalimani unaofanyika katika makongamano au mikutano mbalimbali. Mara nyingi
aina hii ya ukalimani inafanyika katika mikutano ya kimataifa.
Ukalimani wa Mahakama.Aina hii
hufanywa na wanasheria katika mahakama za ngazi mbalimbali. Pia huitwa
ukalimani wa kisheria.
Ukalimani wa Kitabibu. Huu ni ukalimani
ambao unafanyika mahali ambapo matibabu yanapatikana, kwa kiasi kikubwa aina
hii ya ukalimani inafanyika katika hospitali kubwa.
Ukalimani wa Habari/katika vyombo vya habari; Huu ni ukalimani
unaofanywa katika vyombo mbalimbali vya habari, hususani redio na televisheni
ili kuiwezesha hadhira lengwa iweze nayo kuelewa matangazo yanayotolewa kwa
lugha chanzi.
Ukalimani Sindikizi. Katika aina
hii ya ukalimani, mkalimani hufuatana na mtu au kikundi cha watu katika safari
au katika usaili au mahojiano. Mfano, wafadhili wanapoenda kuzindua miradi
waliyofadhiri katika mataifa ambayo yanatumia
lugha ambayo ni tofauti na wanayozungumza, hususani vijijini lazima
waambatane na mkalimani anayefahamu lugha ya wakazi wa pale pamoja na lugha ya
mfadhili.
Kigezo cha Muundo au Mfumo wa Lugha.
Katika kigezo
hiki tunapata aina mbili za ukalimani.
Katika kigezo hiki lugha inayotumika katika ukalimani inaweza ikawa lugha ya
kusema/kuzungumza na lugha ya alama.
(i)
Ukalimani
andamizi (ii) Ukalimani mtawilia
Ukalimani Mfululizo/Andamizi/sambamba. Ni aina ya
ukalimani ambao mkalimani huzungumza takribani sambamba na mzungumzaji wa lugha
chanzi.
Ukalimani huu
ulifanyika kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Nurenberg, ambapo lugha kuu
rasmi za kazi zilikuwa nne. Lugha hizo zilikuwa Kijerumani, Kiingereza,
Kifaransa na Kirusi. Tangu wakati huo mahitaji ya ukalimani yamekuwa
yakiongezeka kwa kiasi kikubwa.
Sifa za ukalimani andamizi.
ü Katika ukalimani
andamizi mkalimani anapeleka ujumbe kwenda lugha lengwa kwa haraka sana
iwezekanavyo kama anavyouchukua kutoka lugha chanzi, huku mzungumzaji wa lugha
chanzi akiendelea kuzungumza.
ü Mkalimani huketi
katika chumba maalum cha ukalimani (booth), ambacho hakipitishi sauti (sound
proof).
ü Mkalimani
huzungumza kwa kutumia kipaza sauti huku akimwona na kumsikia mzungumzaji wa
lugha chanzi kupitia visikizio.
ü Hutumika katika
makongamano ya kimataifa.
ü Mashine ya
kuhamishia ujumbe hutumika katika ukalimani andamizi.
ü Aina hii ya ukalimani inahitaji usikivu na
umakini wa hali ya juu.
ü Mara nyingi
wakalimani hubadilishana kila baada ya dakika 20 hadi 30 ili kupeana nafasi ya
kupumzika.
ü Aina hii ya
ukalimani hutumiwa sana na vyombo vya habari mfano redio na runinga.
Faharasa
Ukalimani
andamizi ni mbinu inayotumika katika ukalimani wa lugha ya alama. Hapo
inapatikana aina nyingine ya ukalimani ambao ni ukalimani wa viziwi.
Udhaifu wa aina hii ya ukalimani.
ü Njia hii ni
hatari sana wakati mwingine mkalimani asiposikia vizuri anaweza kuacha maneno
fulani ama kujitungia ili kufidia ujumbe uliompita.
ü Mkalimani
anakosa uhuru wa kukalimani atakavyo ili kuendana na kasi ya mnenaji chanzi.
Ukalimani mtawalia( Fuatishi). Hii ni aina ya
ukalimani ambao mkalimani huzungumza punde tu mzungumzaji wa lugha chasili
kumaliza ujumbe wake wakati mwingine hata kama hajamaliza ujumbe wake, baada ya
mazungumzo ya lugha chanzi hutulia kwa sekunde chache ili kumpisha mkalimani
kufasili ujumbe.
Vigezo vya ukalimani mtawalia
·
Mara
nyingi mzungumzaji wa lugha chanzi na mkalimani huwa wamesimama au kuketi
sehemu moja.
·
Hutumika
sana katika masuala ya kijamii mfano masuala ya kidini, mahakamani, n.k.
·
Mkalimani
hupata sekunde chache za kutafakari ujumbe.
·
Wakati
mwingine hupeana kipaza sauti kwa zamu
·
Mkalimani
anahitaji kutumia akili kuhamisha ujumbe bila kupotosha.
Stadi za msingi katika ukalimani
Zifuatazo ni
stadi muhimu katika zoezi la ukalimani:-
i.
Lugha
na mawasiliano mfano kuongea, kusikiliza, kuandika na kusoma
ii.
Stadi
ya kunukuu
iii.
Stadi
ya kumbukumbu
iv.
Stadi
ya kuzungumza hadharani (umahiri wa kuongea vizuri mbele ya hadhara).
Dhima ya ukalimani.
Ukalimani
ni daraja linalounganisha watu wanaotumia lugha tofauti. Mfano, watu wanaotumia
Kiswahili huweza kuunganishwa na watu wanaozungumza Kifaransa kwa msaada wa
mkalimani.
Soko
la ajira, watu mbalimbali hufanya kazi ya ukalimani katika mataifa mbalimbali
hivyo hujipatia kipato na kuboresha hali zao za kiuchumi.
Ukalimani
hunufaisha katika kueneza dini ulimwenguni. Mfano watu hutoka katika mataifa
mbalimbali kwa ajili ya kueneza neno la Mungu, hivyo basi wakalimani huchukua
jukumu la kufikisha ujumbe kwa walengwa kwa kufasiri ujumbe wa maneno kwenda
kwenye lugha zao.
Ukalimani
hutumika katika matangazo ya kibiashara na masuala ya michezo. Lengo kuu ni
kufikisha ujumbe kwa wasioelewa lugha chanzi. Mfano hivi sasa matangazo ya
mpira hususani ligi kuu ya mpira wa miguu nchini Uingereza utakuta yanatangazwa
katika lugha mbalimbali tofauti na ilivyokuwa zamani. Pia taarifa mbambali za
matukio duniani yanayoripotiwa na vyombo vya habari vya mataifa ya Ulaya,
matangazo hayo hukalimaniwa katika lugha mbalimbali hususani Lugha za kiafrika
na kurushwa hewani ili mataifa yao wapate habari ile ile.
Ukalimani husaidia kufikisha ujumbe kwa
watu wasiojua kusoma lugha tofauti. Hapa ndio tunaona tofauti kubwa kati ya
tafsiri na ukalimani, ukalimani haubagui mtu yoyoye anapata ujumbe sharti awe
na uwezo wa kusikia tu lakini tafsiri sharti ujue kusoma
Ufanano baina ya tafsiri na ukalimani
Tafsiri na
ukalimani ni taaluma mbili tofauti zinazolandana na kutofautiana katika
vipengele kadha wa kadha. Vifuatavyo ni vipengele vinavyolinganisha taaluma
hizi mbili ya tafsiri na ukalimani.
Lugha. Taaluma zote mbili zinahusisha lugha
katika kulikamilisha kusudio lake. Tafsiri hutumia lugha ya maandishi wakati
ukalimani hutumia lugha ya mazungumzo. Lakini kwa ujumla taaluma zote zinatumia
lugha.
Vijenzi. Ukalimani na tafsiri taaluma hizi zote
hujengwa na vijenzi vyake ambavyo ni matini chanzi, matini lengwa, hadhira,
lugha n.k.Vijenzi hivi ni lazima viwepo ndipo uhawilishaji uweze kufanyika.
Changamoto. Changamoto za tafsiri na ukalimani
zote karibu zinafanana kwa mfano changamoto ya tofauti za kiisimu, tofauti za
kimazingira, tofauti za kiitikadi na dini, tofauti za kitamaduni. n.k.
Dhima. Hiki ni kigezo kingine
kinacholinganisha taaluma ya tafsiri na ukalimani. Majukumu ya tafsiri
yanafanana kabisa na majukumu ya ukalimani, mfano wa baadhi ya kazi ya tafsiri
na ukalimani ni kukuza lugha, kuendeleza na kueneza utamaduni, kuunganisha watu
wa jamii tofauti.
Sifa. Kuna baadhi ya sifa za tafsiri na
ukalimani zinashabihiana kiundani kabisa baadhi ya sifa zinazofanana ni;
taaluma zote hutumia lugha mbili katika zoezi zima la uhawilishaji, mkalimani
au mfasiri lazima ajue utamaduni wa lugha lengwa na chanzi vizuri, mfasiri na
mkalimani hawatakiwi kuegemea upande wowote, pia lazima wote wawe wachapakazi
na kujituma.
Nidhamu na Maadili. Kwa upande wa kipengele hiki
tutajikita zaidi kwa mfasiri na mkalimani kwa sababu wote maadili yao huwa
yanafanana sana, hii ni kwa sababu taaluma hizi zinauhusiano wa karibu sana.
Baadhi ya maadili anayotakiwa kuwa nayo mkalimani au mfasiri ni ;-
ü Lazima ajitume na kufanya kazi kwa bidii.
ü Awe mwenye kujua
majukumu yake na taratibu za kazi.
ü Ushirikiano na
mshikamano kwa wafasiri wenzake.
ü Lazima awe mwaminifu kwa mteja wake na matini
anayoitafsiri pia. Asiwe na upendeleo wa aina yoyote.
Gharama. Taaluma hizi zote zinaambatana na gharama
lukuki mfano, ukalimani katika mikutano ya kimataifa, wakalimani mbalimbali
hufasiri lugha mbalimbali ili kuwezesha mawasiliano.Pia tafsiri mara nyingi
hutozwa gharama kwa kuhesabu kurasa au maneno yaliyotafsiriwa.
Utofauti baina ya tafsiri na ukalimani
Utofauti kati ya
tafsiri na ukalimani pia unajidhihirisha katika vipengele vifuatavyo;-
Maana,kama ilivyo taaluma ya tafsiri
hujishughulisha na upelekaji wa mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha
chasili kwenda lugha legwa. Ilhali, ukalimani ni zoezi la kuhamisha ujumbe ulio
katika mazungumzo kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
Mfumo wa lugha. Lugha inayotumika katika
tafsiri ni lugha ya maandishi, hivyo basi kazi inayofasiriwa sharti iwe katika
maandishi lakini, katika ukalimani lugha inayotumika ni ya mazungumzo ya mdomo, muda mwingine huambatana na ishara.
Aina za tafsiri na ukalimani, kwa upande wa
tafsiri tuna aina nne kuu za tafsiri ambazo ni; tafsiri ya neno kwa neno, sisisi , maana na mawasiliano. Kwa upande
wa ukalimani tuna vigezo viwili, kigezo cha kwanza ni mazingira ya zoezi
linapofanyika, hapa tunapata ukalimani wa kitabibu,
ukalimani wa makongamano, ukalimani sindikizi, ukalimani wa kitaaluma,
ukalimani wa kijamii, ukalimani wa habari au vyombo vya habari n.k. Kigezo
cha pili ni muundo na mfumo wa lugha hapa tunapata ukalimani andamizi na ukalimani mtawalia.
Wahusika, wahusika wakuu hapa ni mkalimani na mfasiri,
katika taaluma ya tafsiri mhusika mkuu anayeshughulikia mchakato mzima ni mfasiri
na katika ukalimani anayesimamia shughuli zote ni mkalimani mwenyewe.
Hadhira, kwa upande wa tafsiri hadhira lengwa
hapa ni wale tu wanaojua kusoma na kuandika kwani ndio pekee watakaoweza
kung’amua kile kilichoandikwa licha ya matini kuandikwa kwa lugha
wanayoizungumza, ilhali hadhira kwa upande wa ukalimani si lazima wajue kusoma
wala kuandika, kitu kikubwa kwao ni kusikia na msaada wa kuona matendo ya
mkalimani ilimradi lugha inayotumika wanaifahamu.
Ukongwe, taaluma ya ukalimani ni kongwe sana na
imedumu kwa muda mrefu lakini, taaluma ya tafsiri imeibuka tu baada ya
kugundulika kwa maandishi.
Muda,
mchakato wa tafsiri unachukua muda mwingi sana kutokana na hatua zake zinazopitiwa
kama vile maandalizi, uhawilishaji,
usawidi wa rasimu ya kwanza, udurusu wa rasimu ya kwanza, kusomwa rasimu ya
pili na mtu mwingine na mwisho kabisa usawidi wa rasimu ya mwisho. Lakini
ukalimani unaweza kufanyika ndani ya siku hata masaa. kwa upande mwingine
mkalimani ana muda finyu sana katika kujiandaa lakini mfasiri ana kuwa na muda
wa kutosha kujiandaa.
Maswali ya ziada
1. Kwa kutumia
mifano fafanua dhana zifuatazo kama zinavyotumika katika tafsiri
i.
Tafsiri
ii.
Ukalimani
iii.
Ukafsiri
iv.
Fasili
v.
Kurudufu
2. Linganisha na
linganua taaluma ya tafsiri na ukalimani.
3. Mchakato wa
tafsiri hauna mwenyewe bali una hatua zenyewe. Jadili.
4. Jadili vigezo
ya mfasiri kabambe ili kupata tafsiri muluwa.
5. Kwa kutumia
mchoro fafanua mbinu nne (4) za tafsiri.
6. Tafsiri na
ukalimani hutofautiana kimaana lakini zinalingana kimajukumu.
7. Jadili
uhusiano uliopo baina ya tafsiri, ukalimani na taaluma zingine.
8. Tafsiri ni
zoezi la uhawilishaji wa ujumbe na si ufananishaji wa maneno. Jadili
9. Jadili dhima tano
za tafsiri katika fasihi linganishi.
10. Tofautisha
kati ya ukalimani andamizi na ukalimani mtawalia.
11. Jadili asili
na chanzo cha ukalimani.
13. Maendeleo ya
tafsiri yamepitia vipindi mbalimbali. Fafanua dai hili kwa mifano muafaka.
14. Jadili vizingiti
vya tafsiri katika muktadha mbalimbali.
15. Fafanua sifa
nne za msomaji wa pili wa rasimu ya pili ya tafsiri.
16. (a) Nini maana ya ukalimani?
(b) Fafanua vigezo vya mkalimani bora
17. Eleza
shughuli tano zinazojitokeza katika hatua ya urudusu wa rasimu ya kwanza ili
kuunda rasimu ya pili.
18. Kwa kutumia
mifano jadili ukale wa taaluma ya tafsiri.
20. Kwa kutumia
mifano ainisha matini kwa kigezo cha dhima kuu za lugha.
21. Kwa usaidizi
wa mchoro fafanua aina nne za tafsiri.
22. Fafanua
dhana zifuatazo kama zinavyotumika katika taaluma ya tafsiri.
(a) matini pokezi
(b) tafsiri pana
(c) tafsiri finyu
(d) jamii ulumbi
(e) matini asili
23. Chanzo cha
ukalimani ni jamiiulumbi. Jadili
24. Badili
sentensi zifuatazo kwenda kwenye kiswahili
i. You can not teach an old dog new
tricks.
ii. Like father like son.
(iii)Clothes don’t make the man.
iii.
As you sow, so you shall reap.
iv.
All
good things come to at a straw.
v.
Action
speak lauder than words.
vi.
A
burnt child dreads fire.
vii.
A
bird in the hand is worth two in the bush.
25. Mfasiri ni
msaliti. Jadili
26. Thibitisha
kauli hii “kwa nini wafasiri wengi wanakosa vigezo vya kuwa wafasiri bora”
27. Tofautisha
kati ya ukalimani sambamba na ukalimani mtawalia. Hoja tano.
28. Kwa kutumia
hoja tano (5) fafanua mbinu bainifu za mfasiri
bora katika kazi ya kufasiri matini mbalimbali.
29. Tafsiri ni
mchakato, bainisha hatua muhimu za mchakato wa tafsiri.
30. Kwa mifano
kuntu, fafanua kingo zinazomfanya mfasiri kukosa tafsiri toshelevu.
31. Mfasiri
anapojaribu kupiga hatua katika kazi yake anakutana na miba zinazomchoma na
kuathiri ufanisi na kusababisha kuibuka na tafsiri tenge. Jadili
32.
Taaluma ya
tafsri na ukalimani ni mapacha wanaofanana zaidi. jadili
33. Taaluma ya tafsri na ukalimani ni
mapacha wasiofanana. Jadili
34. Kwa
kutumia mifano fafanua mikururu ya taaluma ya tafsiri.
35. “Taaluma ya tafsri ni zoezi la
uhawilishaji wa ujumbe kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa”.Fafanua mambo
ya msingi yanayopatikana katika fasili hiyo.
KWA MSAADA ZAIDI WA
MAKALA KAMILI YA TAFSIRI NA UKALIMANI PAMOJA NA MAKALA ZINGINE. USISITE
KUWASILIANA NASI:
Mtila bahati
Barua pepe: bamtila@gmail.com
Blog: mtilabahati.blogspot.com
Rununu: 0675975756/0683797770
Dar- es- salaam
Mpunda H. Muhidini
Barua pepe: muhidinimpunda@gmail.com
Rununu: 0656 984 873/0692 468 788
Dar- es- salaam
Good notes , congratulations I learned something new. Thanks
ReplyDeleteNisaifieni ubora na udjaifu wa ukalimani kimuundo na kimawasiliano
ReplyDeleteNisaidie uhusiano baina ya tafsiri na ukalimani na taaluma zingine
ReplyDeleteNisaidie sifa tank za mkalimani wa lugha ya alama
ReplyDeleteNisaidie uhusiano wa tafsiri na matawi mengine ya isimu
ReplyDelete