SWALI:
Neno na sentensi ni vipashio vikuu
katika sarufi mapokeo. Eleza kinaganaga aina ya maneno na sentensi kwa mujibu
wa sarufi hiyo.
Sarufi
mapokeo
Kwa mujibu wa Khamisi na Kiango
(2002), sarufi mapokeo ni sarufi ya
kale, wataalamu wanaohusishwa na mkabala huu walijitokeza kuanzia karne ya 5 Kabla
ya Kristo na katka karne ya 18 na 19 Baada ya Kristo, wataalamu hao ni kama
Plato, Aristotle, Panin na Protagoras ambao walijihusisha na lugha kwa kutaka
kujua asili yake ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa asili ya maumbo, hususani
walitaka kujua asili yake ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa asili ya maumbo,
hususani walitaka kujua kama lugha ni tukio la kimaumbile au tukio la unasibu.
Massamba na
wenzake (2009) wanaeleza kwamba sarufi mapokeo zilikuwa ni sarufi
elekezi ambazo zilisisitiza kanuni na nini cha kusema na wajua lugha. Watu
wasiojua kanuni za lugha wanapaswa kujifunza kutoka kwa wanaojua sarufi ya
lugha. Wanaendelea kusema kuwa wanaojua lugha hupaswa kutunga kanuni za sarufi.
Waasisi wa sarufi mapokeo walikuwa ni
wanafalsafa wa Ugiriki. Katika kipindi hiki sarufiilshughulikiwa sambamba na
falsafa, dini, fasihi, balagha na mantiki. Waasisi hao ni Plato na mwanfunzi
wake Aristotle (Matinde, (2012).
Kwa mujibu wa
sarufi mapokeo ni kweli kwamba neno na sentensi ndivyo vipashio vikuu katika
sarufi mapokeo. Vipashio hivi (neno na sentensi) vimefafanuliwa kwa undani na
wanasarufi mapokeo kama tutakavyoona hapa chini.
Aina ya
sentensi kwa mujibu wa sarufi mapokeo
Sentensi ni fungu la maneno lenye uarifishaji
mkamilifu. Sentensi huwa na muundo uliokamilika na hujitegemea kimaana
(Matinde, 2012). Pia Massamba na wenzake (2009:136), wanasema sentensi ni kipashio kikubwa kabisa cha
kimiundo chenye maana kamili. Miundo ya sentensi huhusisha vipashio vingine
vidogo kimiundo.
Kwa mujibu wa Matinde (2012:211), tunaarifiwa
kwamba Plato aligawa sentensi katika sehemu kuu mbili: Mtenda (Subject) na
Kitendwa (Object). Pia Massamba na Wenzake (2009:52) katika SAMIKISA wanaongeza
kwamba uchambuzi huo ulizingatia zaidi uamilifu (kazi) wa faridi au vipashio
mbali mbali katika tungo au sentensi.
Kwa mfano, sentensi “Mama anapika chakula”
aliigawa sentensi hii kama ifuatavyo:
Mama
|
anapika chakula
|
Mtenda
(Subject)
|
Kitendwa
(Object)
|
Kwa mujibu wa Habwe na Karanja (2004:142)
wanasema wanasarufi mapokeo
waliainisha sentensi kwa mujibu wa uamilifu wake. Na baadhi ya makundi ya
uainishaji yaliyojitokeza ni kama yafuatayo:
Sentensi taarifa
(arifu)
Matinde (2012:160), anafafanua kuwa “sentensi
arifu ni sentensi ambazo hutoa taarifa au ujumbe fulani.” Sentensi za aina hii
huishia kwa kituo kikuu/nukta. Mifano ya sentensi arifu:
v Baba amenunua kitabu.
v John anaimba vizuri.
Sentensi
agizi (amrishi): Hizi ni sentensi
ambazo huamrisha au humwagiza msikilizaji kutenda kitendo/jambo fulani.
Sentensi hizi huundwa na kitenzi cha kuamuru. Aghalabu sentensi hizi huwa na
sehemu ya kitendwa (kiarifu) tu. Sentensi hizi huishia na kituo kikuu au
mshangao (Matinde, 2012:160). Kwa mfano:
v Leta hiyo sahani.
v Nenda kapige kelele huko nje.
Sentensi
ulizi (swalifu): Sentensi hizi
huwa zina pengo katika sehemu yake ya taarifa. Hivyo hutaka kupata taarifa
Fulani. Hizi ni sentensi ambazo uamilifu wake ni kuuliza swali. Sentensi
swalifu huishia kwa alama ya kuuliza (?). Kwa mfano:
v Mwanao ana umri gani kwa sasa?
v Ndama amepotea lini?
Matinde (2012:161) ameongeza aina za sentensi
zifuatazo kwa kuzingatia kigezo cha uamilifu wake ambazo ni hizi zifuatazo:
Sentensi
mshangao
Matinde (2012:161) anasema sentensi mshangao
ni sentensi ambazo hudhihirisha mshangao wa msemaji kuhusu jambo au hali
fulani. Sentensi hizi huishia kwa alama ya mshangao. Mifano:
v Juma amefeli!
v Chakula kimeshapikwa!
Sentensi
shurutia
Kwa mujibu wa Matinde (2012:161) anaeleza kuwa sentensi shurutia ni sentensi za
masharti ambazo huundwa na vitenzi viwili. Kitenzi cha kwanza hukamilishwa na
kitenzi cha pili ili kuonesha uhusiano wa masharti. Vitenzi hivi huambikwa
viambishi vya masharti mathalani: -nge,
-ngali, -ngeli, na -ki.
Viambishi hivi ni nguzo ya sentensi shurutia. Kwa mfano:
v Juma angelisoma
kwa bidii angelifaulu mtihani
v Jane angaliimba
angalipata zawadi
Aina za
maneno kwa mujibu wa sarufi mapokeo
Baada ya kuwa tumeona namna sarufi mapokeo
ilivyoshughulikia suala la sentensi kwa kuigawa katika sehemu kuu mbili yaani
kiima (Mtenda) na kiarifu (Kitendwa) na sasa tuone namna wanasarufi mapokeo
walivyojishughulisha na maneno na aina zake kama kipashio kingine cha msingi
kwa mujibu wa kigezo hiki. Massamba na wenzake (2009:54) wanasema aina za
maneno zilikuwa ni nomino, Kitendo (Kitenzi), sifa (kivumishi), advebo
(kielezi) n.k. (maneno yaliyowekwa kwenye mabano ni istilahi za siku hizi).
Kwa mujibu wa Matinde (2012:211-212) anaeleza kuwa mara baada ya Plato kugawa sentensi kugawa sentensi
katika sehemu kuu mbili mtenda (Subject) na kitendwa (Object), Aristotle aliweza kwenda mbali zaidi ya
kazi ya mwalimu wake Plato kwa kugawa sentensi katika sehemu kuu tano, ambazo
ni; Nomino, Kitenzi, Kivumishi, Kiunganishi,
na Kielezi.
Matinde (2012:212) anaendelea kueleza kuwa miaka 100
Kabla ya Kristo mwanasarufi Myunani Dionysus Thrax aliandika kitabu cha sarufi
cha awali kabisa ambacho kiliitwa Techne
Grammatike (The art of Grammar). Dionysus Thrax aliainisha sehemu saba za
sentensi ambazo ni; Nomino, Kitenzi,
Kivumishi, Kiwakilishi, Kiunganishi, kielezi, na Kiingizi.
Pia Habwe
na Karanja (2004:131) wanasema wanasarufi mapokeo waliainisha maneno kutokana
na kazi ambazo maneno hufanya katika uundaji wa sentensi. Maneno haya
yameainishwa katika makundi tofauti kulingana na maana na utendaji kazi wake.
Uainishji wa awali wa aina hii ulifanywa na wanasarufi
mapokeo ambao walitambua aina
mabalimbali za maneno walizoziita kategoria
za maneno.
Baadhi ya kategoria walizotambua ni: Nomino, Vitenzi, Viwakilishi, Vivumishi,
Vielezi, Vihusishi, Viunganishi, Vihisishi, Vionyeshi, Vibainishi na
kadhalika.
Nomino: Kwa mujibu wa sarufi mapokeo ni neno la kutaja
vitu- yaani ni majina ya vitu. Hivyo majina nomino hutaja majina ya vitu, watu,
hali, mahali, vyeo, na dhana. Baadhi ya wanasarufi huita nomino majina. Mifano
ya nomino ni kama vile Tanzania, Utundu, Mtoto, Kisu, Malaika na nyinginezo.
Mfano: Baba
analima
Viwakilishi:
Ni maneno ambalo hutumiwa kusimama
badala ya nomino katika sentensi. Viwakilishi pia hujulikana kwa jina la
pronomino. Mifano ya viwakilishi; Wapi unaenda? Neno wapi ni kiwakilishi kiulizi, aina
nyingine ya viwakilishi ni viwakilishi nafsi, viwakilishi vimilikishi,
viwakilishi vya idadi, viwakilishi vya jumla na kadhalika.
Vivumishi: Vivumishi hueleza habari ya kitu au mtu
kikionyesha jinsi mtu au kitu kilivyo. Kisintaksia kivumishi ni neno linalotoa
sifa ya neno au kifungu cha maneno, aghalabu nomino na viwakilishi vyake.
Mifano; Mzee mrefu amewahi.
Kitabu kizuri kimepotea.
Vitenzi: Ni maneno ambayo huwakilisha kitendo.Mbaadu
(1985) anaeleza kuwa vitenzi kama maneno yoyote yanayoonyesha mambo
yanayofanywa na watu, wanyama, au vitu katika wakati fulani. Pia vitenzi
hueleza hali Fulani za watu, vitu, na matukio. Vitenzi ni kama vile imba,
cheza, lima, sema, soma na kadhalika.
Mfano; Mama analima shamba.
Watoto wanaimba nyimbo zao vizuri.
Vielezi: Ni maneno au fungu la maneno ambalo huongeza maana
ya kitendo. Ni maneno yanayofafanua vitenzi, vivumishi, na vielezi
vingine. Mifano ya vielezi ni kama vile sasa hivi, ovyo ovyo, asubuhi na mapema.
Mfano; Mwanafunzi ameondoka sasa hivi.
Jack anacheza vizuri.
Vihusishi: Ni neno aukundi la maneno yanayohusisha sehemu
mbili au zaidi za sentensi. Huonesha uhusiano baina ya kitu na kingine au mtu
na mwingine kama wahusika katika sentensi. Mifano ya vihusishi ni maneno kama
vile katika, juu ya, kwa, hadi na
kadhalika.
Mfano; Omari anacheza juu ya kitanda.
Mtoto anakula kwa kijiko.
Viunganishi
Ni maneno ambayo huunganisha maneno au mafungu
ya maneno. Viunganishi huweza kuunganisha maneno na maneno, au maneno na
vikundi vya maneno na vikundi vingine vya maneno. Mifano ya maneno ambayo ni
viunganishi ni kama vile na, kisha,
na kadhalika.
Mfano; Juma na Ali wanasoma. (Neno kwa neno).
Ali alikwenda maktaba kisha akasoma
jarida. (kishazi na kishazi)
Vionyeshi
Kwa mujibu wa Kapinga (1983) vionyeshi ni maneno
yanayoonyesha ujirani wa kitu kwa kukihusisha na kitu kingine. Vionyeshi pia
vimerejelewa kama viashiria. Mifano ya vionyeshi ni kama huyu, wale, hao na vinginevyo.
Mfano; Wale
wanakuja.
Hao ni wazuri.
Vihisishi: Ni aina ya maneno ambayo huonyesha hisia kama
vile hali ya kufurahi, uchungu, kushangaa, kushtuka na kadhalika. Awali
vilijulikana kama vishangao lakini hii haikutosheleza jukumu la vihisishi kwa
sababu vishangao ni aina moja tu ya vihisishi yaani vile vinavyoonyesha
mshangao tu. Mifano ya vihisishi ni kama alhamdulillahi!,
Mungu wangu! Ebo! Simile! Lahaula! na vinginevyo.
Mfano wa kihisishi; Mungu wangu! Amepotea?
Vibainishi: Kategoria hii haipokatika lugha ya Kiswahili.
Huweza kupatikana katika baadhi ya lugha ikiwemo lugha ya kiingereza.
Vibainishi hutumiwa pamoja na nomino.
Kwa mfano:
The student ate all the food, An elephant is a wild animal.
A book is a good thing to have.
Hivyo ndivyo ambavyo wanasarufi mapokeo
walivyoweza kuainisha maneno na sentensi ambavyo ndivyo vipashio vya msingi vya
lugha kwa kuzingatia kigezo hiki cha sarufi mapokeo. Kikubwa ni kwamba wao
katika uainishaji wao waliegemea zaidi uamilifu wa tungo hizo yaani kazi ambazo
maneno na sentensi hufanya.
MAREJELEO
Habwe, J. & Karanja,
P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili.
Nairobi: Phoenix Publishers Ltd
Khamis, A. M. & Kiango,
J. G. (2002). Uchambuzi wa Sarufi ya
Kiswahili. Dar es salaam:
TUKI.
Massamba, D. P. B. na wenzake (2009). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu
(SAMIKISA):
Sekondari na Vyuo.
Dar es salaam: TUKI.
Matinde , R. S. (2012).
Dafina ya lugha isimu na nadharia: Kwa
Sekondari, Vyuo vya Kati na
Vyuo Vikuu. Mwanza:
Serengeti educational publishers