14 Jul 2025

 


Kuwasiliana kwa njia ya maandishi

Dhana  ya mawasiliano kwa njia ya maandishi

Mawasiliano kwa njia ya maandishi ni aina ya mawasiliano ambayo huhusisha  matumizi ya matini mbalimbali kama vile barua, hotuba, risala, kumbukumbu za vikao, kifungu cha habari  na insha.

Mambo yakuzingatia katika kufikisha ujmbe wa maandishi

i.      Mwandishi anapaswa kuzingatia ufasaha wa lugha anayotumia ili msomajia aweze kuelewa ujumbe uliokusudiwa

ii.    Mwandishi anapaswa kuzingatia matumizi ya lugha  fasaha  kwani yatamsaidia msomaji kuuelewa  na kukuza lugha inayohusika kwa ufasaha

iii.  Mwandishi anapaswa kutumia msamiati sahihi unaoendana na muktadha   wa mada inayohusika

iv.  Mwandishi anapaswa kuzingatia uhusiano sahihi wa maneno ili kujenga sentesi zinazoeleweka kwa msomaji

v.    Mwandishi anapaswa kuzingatia matumizi sahihi ya viunganishi  na tahajia

vi.  Mwandishi anapaswa kuzingatia alama za uandishi  vyema ili maudhui yaliyokusudiwa yaweze kumfikia msomaji.

 

 

 

 

Taratibu za Uandishi

Taratibu za uandishi ni alama na mpangilio wa maneno yanayo mwongoza mwandishi kuandika kwa usahihi. Ili habari iweze kuwa nzuri, inayoeleweka vizuri kwa wasomaji, mwandishi hana budi kutumia alama. Alama hizi humsaidia msomaji kujua wapi pa kupumzika, kuuliza swali, kushangaa, n.k. Alama zifuatazo hutumiwa katika uandishi:

Nukta (.)

(a) Hutumika kukamilisha sentensi

Mfano:Mama anapika jikoni.

(b)Hutumika kuonesha ufupisho wa maneno

Mfano:n.k (nakadhalika), k.m (kwa mfano), S.L.P (sanduku la posta).

(c) Hutumika kuonesha vipimo mbalimbali katika desimali

Mfano:     saa 3.45, meta 92.3, kilogramu 8.2

 

Mkato (,)

(a) Hutumika kuweka pumziko fupi katika sentensi

Mfano:     Alipofika shuleni alipokelewa na Ashura, Musa na Mwalimu Tino.

(b)Hutumika kutenga maneno yaliyo katika orodha

Mfano:     Ninunulie kalamu, kitabu, ufutio na karatasi

(c) Hutumika kuonesha sehemu mbili za sentensi zilizo kinyume

Mfano:     Aliye juu, mngoje chini

                Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

(d)Hutumika kabla ya alama za mtajo.

Mfano:     Mwalimu Sawaka alisema, “leo nitawafundisha”

(e) Hutumika kuonesha vyeo, anuani au maskani baada ya jina la mtajwa.

Mfano:     Moses Okelo , Mkurugenzi wa Halmashauri-Nzega.

(f)  Hutumika badala ya viunganishi

Mfano:     Unacheza au huchezi?

Usipotaka kutumia kiunganishi au unaweza kuandika

                Unacheza, huchezi?

(g) Hutumika kabla na baada ya vifungu vya maneno vielezavyo maneno yaliyotangulia.

Mifano:    Helasita, shule ya mfano Tanzania, huwezi kuifananisha.

                Mihambo, mwalimu pekee wa somo la Kiswahili, aliyekutana na Rais Trump Marekani.

(h)                Hutumika mbele ya vifungu vya vielezi vinavyokaa mwanzoni mwa sentensi.

Mifano:    Kimyakimya, aliingia ndani huku akilia.

                Kwa mbwembwe nyingi, alianza kupigana.

 

 

 

 

 

Nukta mbili/Nukta pacha (:) 

(a) Hutumika kuashiria vitu vilivyo katika mfululizo au orodha.

Mfano:     Nilimletea mama: nguo, viatu, gauni na kitenge.

(b)Hutumika katika maandishi ya kitamthiliya.

Mifano:    Mwalimu Masawe: (kwa upole)hamjambo wanafunzi

                Wanafunzi: Hatujambo shikamoo mwalimu.

                Mwalimu Masawe: Marahaba! Kaeni.

(c) Hutumika kutenganisha saa, dakika na sekunde.

Mifano:    Saa 9:45, saa 2:28:10

                Saa 2:20:10, saa 12:00 n.k.

(d)Hutumika kuonesha uwiano baina ya namba.

Mfano:     8:7, 26:20, 7:6

(e) Hutumika kutenganisha tarakimu kama vile za maandiko matakatifu.

Mifano:    Yohana 3:16-19

                Matendo ya Mitume 8:1-3

 

Nukta Mkato (;)

(a) Hutumika kuunga tungo mbili zenye sifa zinazolingana lakini zisizo na kiunganishi.

Mfano:     Wengine wanacheka; Wengine wanalia.

                Jackline Tiganga anasoma;Ghati anaandika

 

(b)Hutumika ili kuonesha pumziko la muda mrefu zaidi katika kusoma kuliko unapotumia mkato.

Mifano:    Mwalimu Neema anafundisha vizuri; anatamani kutuona tukifaulu vizuri.

Triphonia anapenda sana kuchora; inaonyesha jinsi atakavyokuwa mchoraji wa kimataifa.

 

 


Kistari (-)

(a) Hutumika kuonesha neno limekatwa kwa kuwa limefika ukingoni mwa karatasi wakati bado linaendelea katika mstari unaofuata. Kwa kawaida neno lenye silabi moja halikatwi, huandikwa lote mwishoni mwa mstari au kama nafasi haitoshi, mwanzoni mwa mstari unaofuata.

Mifano:    Alipofika hapa ali-

pewa zawadi

 

(b)Hutumika kuunga maneno mawili.

Mfano:     Askari –kanzu, Idd-el-fitri

                Kipima-pembe

                Dar-es-Salaam

(c) Hutumika kuendeleza sauti

Mfano:     A-a-a-a-a

                Lo-o-o-o

(d)Hutumika kuunga sentensi mbili, sentensi ya pili ikiwa ni ufafanuzi wa sentensi ya kwanza.

Mfano:     Kulikuwa na kusanyiko kubwa sana uwanjani- wanaume, wanawake na watoto walihudhuria.

(e) Hutumika badala ya nukta mbili.

Mfano:     Nichukulie- shati, gauni na koti.

 

 

Mabano( )

(a) Hutumika kuonesha maana ya ziada katika sentensi.

Mfano:     Rais Mstaafu wa awamu ya nne(Jakaya Kikwete) ni mtu hodari.

                Nchi yangu (Tanzania) ina demokrasia makini.

 

 

 

 

 

Alama ya kuuliza (?)

(a) Hutumika badala ya nukta au alama ya kushangaa ili kufunga sentensi zinazouliza maswali. Baada ya alama hii, sentensi inayofuata huanza kwa herufi kubwa.

Mfano Mama yuko wapi? Mbona haonekani?

 

(b)Hutumika kuuliza swali

Mfano: Wewe unaitwa nani?

 

 

Alama ya kushangaa (!)

(a) Hutumika baada ya neno au usemi wa kushangaa, kushtuka, huzuni au uchungu. Baada ya alama hii kutumika, sentensi inayoanza huanza kwa herufi kubwa.

Mfano:     Loo! Mtoto wewe huna adabu

                Kumbe amefariki!

 

(b)Hutumika wakati wa kusisitiza jambo kama vile kero, kubeza, utani n.k.

Mfano:     Ona ulivyo mjinga!, Ondoka hapa wewe kima!

 

Alama za mtajo (“…..”)

(a) Hutumika katika kukariri maneno yaliyosemwa au kuandikwa na mtu mwingine.

Mfano:     Mwalimu alisema, “Wote mnastahili zawadi nono”

                Juma alijibu, “Hata mimi ninastahili zawadi nono”

 

(b)Hutumika kuonesha maneno ya lugha ya kigeni

Mfano:     Hilda Fundi ni “Intelligent”

                Mwalimu hakufanya “fair”

 

 

 

(c) Hutumika kubainisha misimu, maneno yasiyokubalika katika lugha inayoandikwa.

Mifano:    Amekutwa akitumia “ngada” chooni.

Timu ya Simba “walitoswa” na wenyeji wao huko Manungu.

 

 

Ritifaa (‘) Kibainishi

(a) Hutumika kutofautisha ng na ng’ katika maneno.

Mfano ng’ombe, ng’arisha, ng’ang’ania, ng’aa n.k.

 

(b)Hutumika kuonesha kwamba herufi fulani imeachwa hasa katika ushairi.

Mfano:     ‘mejaribu jongea ndege awe mkononi.
                 Nimejaribu jongea ndege awe mkononi.

 

 

Mstari wa mshazari ( / )

(a) Hutumika katika nambari ya kumbukumbu

Mfano:     NA: PT / BT / 60

 

(b)Hutumika katika kutenga tarehe, mwezi na mwaka.

Mfano:     6/8/2022

 

(c) Hutumika badala ya neno au.

Mfano:     Bw/Bi

                Dawa/chakula

                Nyeusi/nyekundu

                Asubuhi/jioni

 

 

 

 

 

 

Herufi kubwa

(a) Hutumiwa mwanzoni mwa sentensi, baada ya nukta, baada ya alama ya kushangaa au alama ya kuuliza.

Mfano:     Tanga ni mkoa ulioko Kaskazini mwa nchi yetu. Mkoa huo unasifika kwa jambo gani? Jambo la kwanza ni kilimo cha mazao ya biashara.

 

(b)Hutumika katika kuandika nomino za pekee kama majina ya watu, miji, vyeo na Mungu.

Mfano:     Kajuna – jina la mtu

                Arusha – jina la mji

                Rais-jina la cheo au wadhifa

 

(c) Hutumika katika kuandika herufi ya kwanza ya kauli iliyokaririwa.

Mfano:     “Nitawaadhibu wote,” Mwalimu Lugome alisema.

 

(d)Hutumika katika kuandika vifupi vya majina ya watu, vyama au kampuni.

Mfano:     J.K. T – Jeshi la Kujenga Taifa.

 

(e) Hutumika kutaja majina ya sikukuu, sayari, siku, miezi, pande, dira, majina ya vitabu na mada.

 

 

Nukta katishi (…….)

(a) Hutumika kubainisha mdokezo

Mfano:     Anatuongoza vizuri lakini ………

 

(b)Hutumika kuonesha kuwa kuna maneno yaliyotangulia katika tungo.

Mfano:     …………ndio waliochaguliwa na Rais

 

 

Aya

Ni jumla ya sentensi zinazoeleza wazo moja. Hivyo, mkusanyiko wa sentensi zenye wazo kuu au sentensi zinazolifafanua wazo hilo huitwa aya.

Aya hueleza au kufafanua wazo maalumu, pia hurahisisha kazi ya msomaji kwa kuwa na mawazo yenye mantiki. Aya hupunguza au kuondoa marudio ya mawazo kwa sababu kila aya hubeba wazo moja linalojitosheleza.

Mambo ya kuzingaitia katiika uandishi

i.      Hakikisha unalielewa vyema jambo unaloliandikia. Hii itakusaidia kuandika jambo hilo kwa upana na kufikisha ujumbe kamili kwa jamii iliyokusudiwa

ii.    Fuata mtiririko mzuri wa mawazo  ili kupangalia maudhui vizuri na kufanya yaeleweke kwa msomaji

iii.  Tumia lugha fasaha

iv.  Zingatia alama za uandishi

v.    Hakikisha unamsamiati wa kutosha  utakaokuwezesha  kuandika na kujieleza vizuri

vi.  Akikisha unamifano ya kutosha

Kazi

1.  Andika tena sentensi zifuatazo, ukitumia alama za uandishi zifaazo.

(a) tanga kuna machungwa mengi

(b)unataka kufanya nini

(c) Nilikwambiaje

(d)leo ni tarehe 29 agosti 2022

(e) Mimi ni mwenyeji wa dodoma

(f)  hassani ni bondia mzuri

(g) nenda dukani ukaninunulie mafuta ya kula mafuta ya kupaka na mafuta ya nywele

2.  Tumia ritifaa kusahihisha maneno yafuatayo.

(a) Ngoa

(b)Ngatuka

(c) Ngombe

(d)Ngoka

(e) Ngamua

3.  Tumia herufi kubwa kusahihisha uandishi wa nomino hizi za kipekee.

(a) tanzania

(b)mihambo

(c) ashura

(d)dodoma

(e) holoma

 

4.  Tunga sentensi tano zenye kukata maneno zinapofikia ukingoni mwa karatasi.

5.  Tumia alama za uandishi zifaazo kurekebisha kifungu kifuatacho.

 

namjua mkurugenzi wa shule ya sekondari helasita kwa moyo wake mzuri anapenda kuona sisi wanafunzi tukifanya vizuri kwenye masomo yetu siku moja alipotutembelea shuleni alituuliza je tunataka atuongezee walimu wa somo gani mimi nilijibu pasi kuwatazama wenzangu kiswahili mwezi mmoja baadaye alimleta mwalimu wa somo la kiswahili kutoka jiji la arusha ambaye amekuwa chachu ya mafanikio ya shule ya helasita.

 

6.  Fafanua dhima tatu za aya.

7.  Tumia alama za uandishi zifaazo kusahihisha sentensi zifuatazo.

(a) nilijitahidi kuwa mpole kwa wote mwalimu alisema

(b) niombee ruhusa kwa mwalimu wa zamu joan alisema

(c)  titi la mama ni tamu hata likiwa la mbwa ni shairi zuri sana

(d) mimi napenda kula ugali maharage na nyama

(e)  ninapenda sana kipindi cha azam sports arena

 

Kazi

Chunguza picha ifuatayo kisha jibu maswali yanayofuata.

 

 

 

Picha ya mwanafunzi akiandika insha huku karatasi yake ikionesha kichwa cha insha ni umuhimu wa sensa.

 
 

 


       

 

 

 

 

 

 

Maswali

1.  Mwanafunzi katika picha anafanya nini?

2.  Kipi ni kichwa cha insha anayoiandika mwanafunzi?

3.  Andika majina ya vifaa vyote anavyotumia mwanafunzi kuandika insha.

 

 

 

Dhana ya insha

Insha ni utungo wa maneno kuhusu jambo fulani. Ni mfululizo wa sentensi zinazohusiana na mada inayozungumziwa au kuandikwa. Insha inaweza kuwa ndefu au fupi kutegemeana na kusudi la mwandishi na mada anayoiandika. Insha hugawanywa kwenye vifungu vya maneno vinavyoitwa aya. Kwa kawaida, aya hubeba wazo maalumu.

Muundo wa insha

Muundo wa insha umegawanyika katika sehemu zifuatazo:

1.  Kichwa cha insha

Huandikwa kwa herufi kubwa juu ya karatasi ya kuandikia, huwa katikati juu ya insha. Huandikwa kwa ufasaha na kwa kifupi (muhtasari). Kichwa cha insha hakitakiwi kuwa na maneno mengi, kinatakiwa kisizidi maneno matano(5) wakati mwingine hupigiwa mstari.Kichwa cha insha wakati mwingine pia hujitokeza kikiwa katika wino mzito au uliokoza kwenye baadhi ya maandiko kama vile magazeti.

 

2.  Utangulizi / Mwanzo wa insha

Sehemu hii huzingatia fasiri au ufafanuzi wa jambo linalozungumziwa, uhusiano wake au muhtasari wa insha inayotungwa. Kwa kawaida utangulizi hauzidi aya moja.

 

3.  Kiini cha insha

Hii ndiyo sehemu kuu ya insha. Huzingatia mawazo makuu ambayo hupangwa katika aya zenye mtiririko wa mawazo. Huonesha kwa undani maana ya jambo linalotungwa, kuenea kwake na uthibitisho wake.Sehemu hii huandikwa aya zilizosheheni hoja mbalimbali kuhusu jambo linaloandikiwa insha.

 

4.  Mwisho wa insha (hitimisho)

Ni aya ya mwisho katika insha ambayo huwa na maoni na mapendekezo ya mwandishi kuhusu jambo linalotungiwa insha. Mwisho wa insha hautakiwi kuzidi aya moja.

 

Aina za insha

Kuna aina mbili za insha ambazo ni:

(a) Insha za wasifu

(b)Insha za hoja

 

Katika hatua hii ya kidato cha kwanza tutazungumzia insha za wasifu peke yake na aina nyingine tutajifunza katika madarasa mengine.

 

 

 

 

 

 

 

 

Mambo ya kuzingatia katika kutunga insha

Yapo mambo ya msingi ya kuzingatia wakati wa utungaji insha. Mambo hayo ni haya yafuatayo:

1.  Kuandika kichwa cha insha na maelezo yote kama yapo.

 

2.  Kuandika kwa kufuata taratibu za uandishi na lugha ambayo ni fasaha. Mfano epuka kutumia lugha ya mkato, yaani vifupisho kama vile n.k badala ya nakadhalika, k.m badala ya kwa mfano, k.v badala ya kama vile, ktk badala ya katika. Andika neno lote kama lilivyo, lakini pia unapoandika insha epuka kuandika nambari kwa tarakimu, kwa mfano, kuandika 12 badala ya kumi na mbili. Andika nambari kwa maneno.

 

3.  Andika utangulizi unaovutia makini ya wasomaji au wasikilizaji. Utangulizi ambao hauvutii humfanya msomaji au msikilizaji kuchoka na kutopenda kuendelea kusoma au kusikiliza insha yako.

 

4.  Andika kiini cha insha yako kwa mpangilio unaofaa. Kila wazo kuu liandikwe kwenye aya yake. Mawazo ya aya zote yahusiane.

 

5.  Andika mwisho wa insha unaovutia ili wasomaji wapende kurudia kusoma insha hiyo.

 

Insha za wasifu

Ni aina za insha ambazo huelezea sifa nzuri au mbaya za viumbe mbalimbali kama vile watu, wanyama, ndege, wadudu, mimea, majengo, mahali na kadhalika.

 

Kazi

Tunga insha ya maneno mia tatu (300) kuhusu picha hiyo hapo chini.

 

 

Picha ya Mlima Kilimanjaro

 
 

 

 

 

 

 

 

 


Aina za insha za wasifu

Kuna aina mbili za insha za wasifu.

(a) Insha za wasifu za kisanaa

(b)Insha za wasifu zisizo za kisanaa

 

(a)         Insha za wasifu za kisanaa

Hizi ni aina za insha ambazo hueleza kwa upana kuhusu sifa za watu, wanyama, mahali na vitu kwa kutumia lugha ya kisanaa iliyosheheni tamathali za semi, mbinu nyingine ya kisanaa, taswira, lugha ya kuvutia na matumizi ya semi kama vile methali, nahau, mafumbo, vitendawili na misemo.

 

 

 

 

Mfano wa insha ya wasifu ya kisanaa

MALAIKA SHULE YA MFANO TANZANIA

 

        Helasita ni shule ya mfano Tanzania. Hapa ni mahali ambapo wataalamu mbalimbali na magwiji wa kuunganisha mwili wa binadamu hutengenezwa. Kila anayeingia Malaika hutoka akiwa ubongo wake umenolewa kisawasawa.

        Kuna shule nyingi sana nchini Tanzania, lakini hii ni bora zaidi. Madarasa yake ni makubwa, mithili ya hekalu la Mfalme Suleimani. Ndani ya madarasa kuna vibao vikubwa vilivyo nakshiwa maandishi yanayotoa mwongozo na kanuni za shule, viti vya kukalia ni kama vile wanavyokalia wageni wanaoingia Ikulu pale Magogoni. Upepo ukivuma kila darasa humeza hewa ya kutosha kutoka kwenye maua na miti inayoizunguka shule hii. Achilia hewa safi iingiayo kwenye madarasa, nje ya madarasa yetu kuna bustani maridadi kuliko bustani ya Edeni.

        Katika shule yangu Malaika, tunajivunia uwepo wa walimu mahiri wa masomo mbalimbali, hakika walimu na wafanyakazi wa shule hii ni werevu sana kwani hutuelimisha bila kukata tamaa wakiongozwa na jemedari nambari moja ambaye ni Meneja wa shule yetu. Hakika kila mwanafunzi anajisikia faraja maishani kwani hakuna mwanafunzi ambaye ni mbumbumbu. Wanafunzi wa shule hii ni mafundi wa kutumia ubongo katika kutatua masahibu mbalimbali yanayojitokeza.

        Mambo mengine muhimu ya kujipigia kifua katika shule hii ni majengo matakatifu yaliyotulia kama nguzo zibebazo Msalaba wa Vatikani. Majengo mazuri yaliyokaa kama uyoga hupendezesha shule na kuifanya shule kuwa kitovu cha maarifa. Maabara za kisasa na chumba cha wale wenye kudonoa chombo cha kuandikia huvutia sana, bwawa la kuogelea nalo ni kivutio kikubwa cha watu kutoka Ughaibuni.

        Hata ningepewa mwaka mzima kuielezea shule hii siwezi kumaliza. Nimeangalia afya za walimu, namna wanavyovaa, ngozi zao zilivyo na vinyweleo vya manyunyumanyunyu ni ishara tosha kuwa Mkurugenzi anaupiga mwingi kwenye kuwajali walimu na wafanyakazi wengine. Hii ndiyo Malaika, shule ambayo inapatikana katika jiji la Dar es Salaam, wilaya ya Kigamboni .

 

(b)         Insha za wasifu zisizo za kisanaa

Ni aina ya insha ambazo hutumia lugha ya kawaida na rahisi na ya kueleweka. Insha za aina hii hazina mahadhi ya kisanaa, matumizi ya lugha ya mjazo hayapo kwani mwandishi hutumia lugha nyepesi na kutoa mifano halisi.

 

Mfano wa insha ya wasifu isiyo ya kisanaa.

 

NYERERE KIONGOZI WA DUNIA

 

        Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anabaki kuwa kiongozi wa kipekee sana Tanzania, Afrika na duniani kwa ujumla. Japo alizaliwa kwenye familia ya Uchifu huko Mkoa wa Mara kwa Wazanaki, lakini hakupenda kujikweza.

        Mwalimu aliishi maisha ya kawaida, hakuwa na ulinzi mkali, hakutembelea magari ya thamani na hata hakuwahi kujenga nyumba ya thamani. Kumbuka nyumba yake ya kule Mwitongo, Butiama Mkoa wa Mara alijengewa na serikali baada ya kuomba msaada.

        Aprili kumi na tatu mwaka elfu moja mia tisa na ishirini na mbili ndio mwaka aliozaliwa na mwaka elfu moja mia tisa hamsini na tatu, akiwa kijana wa miaka thelathini na moja, wazee wapigania uhuru wakati huo walimuamini na kumchagua kuwa mwenyekiti wa chama cha siasa cha Tanganyika African Association (TAA).

        Mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka elfu moja mia tisa hamsini na nne kwa kushirikiana na vijana wenzake akina Rashidi Kawawa, Kambona, watoto wa Kleist Sykes, Dossa Aziz na John Rupia ambaye inasadikika ndiye alikuwa anaongoza kwa utajiri kati ya Watanganyika wote wa wakati huo, walipambana kwelikweli na serikali ya Mwingereza.

        Walipambana mpaka waliposhinda kwenye uchaguzi ambao ulisababisha Mwalimu Nyerere kuwa Waziri Mkuu Kiongozi wa kwanza mweusi nafasi aliyoihudumu tangu Septemba mbili, mwaka elfu moja mia tisa na sitini mpaka Mei moja, mwaka elfu moja mia tisa sitini na moja alipoamua kung’atuka baada ya kuona yupo kwenye mfumo wa serikali ya Waingereza.

        Mwaka huo huo, elfu moja mia tisa na sitini na moja, Nyerere alifanikiwa kuongoza mapambano kwa nguvu zaidi na kuudai uhuru kamili wa Tanganyika ambapo Desemba tisa, mwaka elfu moja mia tisa sitini na moja Tanganyika ikawa huru. Bendera ya Uingereza ikashushwa Desemba nane, mwaka elfu moja mia tisa sitini na moja saa tano na dakika hamsini na tisa na bendera ya Tanganyika ikapandishwa Desemba tisa, mwaka elfu moja mia tisa na sitini na moja saa sita kamili usiku

        Baada ya kupata uhuru mwaka elfu moja mia tisa na sitini na moja, Mwalimu Nyerere aliunda Baraza lake la mawaziri lenye mawaziri kumi na moja tu, idadi ndogo kuliko serikali zote zilizofuata. Mawaziri hao walikuwa vijana tupu wenye umri chini ya miaka thelathini na tisa huku Nyerere mwenyewe akiwa na miaka thelathini na tisa.

        Mwalimu Nyerere aliamini sana kuwekeza kwa vijana ukiachilia mbali Baraza lake la Mawaziri kujaa vijana kwa asilimia tisini na tisa, alisukumwa zaidi kwa sababu yeye mwenyewe alianza harakati za kupigania uhuru wa nchi yake akiwa kijana. Huyu ndiye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye dunia nzima inamkumbuka kwa ujasiri wake na uongozi ulio bora.

 

 

 

 

Uandishi wa barua

 

 

 

 

 

 

Picha ya mwanafunzi anaandika barua

 
 

 

 

 

 

 

 

 


Barua ni mojawapo ya njia ya mawasiliano kama ilivyo simu, kadi nakadhalika. Kuna aina nyingi za barua. Baadhi yake ni hizi zifuatazo: Barua za kirafiki, barua rasmi, barua za magazeti, barua za mialiko nakadhalika.

Barua za kirafiki

Hizi ni barua ambazo huandikwa kwa marafiki, wazazi na ndugu wengine. Barua hizi humpa uhuru mwandishi kuandika barua yake akitumia lugha isiyo rasmi (kama anavyopenda). Uhuru huu humpa mwandishi wa barua ruhusa ya kuandika barua yenye urefu anaotaka. Mwandishi wa barua hii na anayeandikiwa huwa wanajuana vizuri kiasi cha kuandikiana barua wakitumia lugha ya kawaida waliyoizoea.

 

Kazi

Utajuaje kuwa barua uliyoandikiwa / uliyoandika ni barua ya kirafiki? Fafanua.

 

Mambo ya kuzingatia wakati wa kuandika barua za kirafiki

1.  Anwani ya mwandishi

Huandikwa juu upande wa kulia wa karatasi. Huwa na muundo wa mshazari, wakati mwingine huwa wima, mkato, kituo na taratibu nyingine za uandishi huzingatiwa.

 

Mfano 

Shule ya sekondari Helasita,

S.L.P 11639,

Dar es salaam.

 
                               

                                                                        Mkao wima.

 

 

 

                                au           

Shule ya sekondari Helasita,

  S.L.P 11639,                          Mkao mshazari

     Dar es salaam.

 

2.  Tarehe ya kuandika barua

Huandikwa chini ya anwani ya mwandishi wa barua  . Lengo ni kumjulisha mwandikiwa lini barua iliandikwa. Tarehe huweza kuandikwa kwa mitindo mbalimbali kama vile:

                      24 Septemba 2022

                      24 – 9 – 2022

                      24 . 9 .2022

                      24 / 9 / 2022

                      Septemba 24, 2022

Baada ya tarehe kuandikwa, mwandishi wa barua aruke mstari mmoja.

 

3.  Mwanzo wa barua

Huanzia upande wa kushoto karibu kabisa na mstari wa pambizo. Maneno yanayoweza kutumika mwanzoni mwa barua ni kama vile; mpenzi baba, mama mpendwa, ndugu mpendwa, shangazi mpenzi, kwako kaka, dada yangu mpendwa. Baada ya mwanzo, aya fupi ya salamu hufuata.

 

4.  Kiini cha barua

Hii ni sehemu muhimu sana katika barua kwani ndio sehemu ambayo mwandishi hueleza lengo lake la kuandika barua. Katika sehemu hii mwandishi huweza kueleza kusudi lake. Mfano kusalimia, kuomba msaada, kutoa pongezi na kadhalika. Kiini kinaweza kuwa na aya moja au zaidi ambayo mwandishi angependa kuwasilisha kwenye barua yake.

 

5.  Mwisho wa barua

Sehemu hii huwa na salamu za maagano. Salamu hizi hutegemea pia uhusiano uliopo baina ya mwandishi na mwandikiwa. Maneno ambayo mara nyingi hutumiwa wakati wa kumaliza barua ni kama yafuatayo:

                      Wasaalamu

                      Wako akupendaye

                      Wako wa moyoni

                      Kwa heri

                      Rafiki yako akupendaye

                      Leo naishia hapa, na kadhalika.

6.  Jina la mwandishi

Sehemu hii ni muhimu sana kwani humsaidia yule anayepelekewa barua kufahamu barua imetoka kwa nani. Iwapo barua imechapwa kwa mashine (taipureta au kompyuta), mwandishi huandika jina lake kamili, kama imeandikwa kwa mkono mwandishi ataandika jina lake kamili au jina moja tu. Endapo barua itazidi ukurasa mmoja, kurasa hizo itabidi zipewe namba.Ikumbukwe kuwa barua za kirafiki hazina kipengele cha Saini ya mwandishi wa barua.

Kielelezo cha muundo wa barua ya kirafiki

 

Anuani ya mwandishi

 

Tarehe

 

Salamu

 

Mwanzo wa barua

 
 

 

 

 

 

 

 

 


   

 

 

 

 

Kiini cha barua

 

 

 

 

Mwisho wa barua

 

Jina la mwandishi

 
 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 


                                    

Mfano wa barua ya kirafiki / kindugu

Shule ya Sekondari Azimio,

  S.L.P 284,

    Arusha.

      26/09/2022.

Baba mpendwa,

        Salamu sana. Habari za siku nyingi? Abigael hajambo? Mama naye hajambo? Mimi ni mzima kabisa na ninaendelea vizuri na masomo yangu hapa shuleni.

        Dhumuni la barua hii ni kutaka kukujulisha kuwa mimi ni mzima na ninaendelea vizuri na masomo yangu japo najisikia mpweke sana kutokana na kwamba sikuzoea kukaa mbali nanyi wazazi wangu.

        Baba, naomba umwambie mama, asisahau kuniombea kwa Mungu ili nifaulu vizuri katika mitihani yangu yote. Naomba pia usisahau kunitumia pesa ya matumizi ili niweze kununua mboga mboga na dagaa kantini hasa siku ya ugali na maharage.

        Kwa leo naishia hapa, wasalimie wote wanaonifahamu hasa majirani zetu wote.

Ni mimi mwanao

Triphonia.

 

 

 
 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 


Kazi

1.  Wewe ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Mawasiliano, S.L.P 145, Morogoro. Mwandikie barua shangazi yako ambaye ni Mkuu wa shule katika shule ya sekondari Mawenzi S.L.P 342 Singida ukimwomba akutumie pesa ya matumizi. Jina lako ni Furaha Falisha.

 

2.  Chora kielelezo cha muundo wa barua ya kirafiki kisha ufafanue umuhimu wa kila kipengele.

 

3.  Andika barua kwa mlezi/mzazi wako ili umweleze siku utakayowasili nyumbani baada ya kumaliza mtihani wako wa mwisho wa mwaka. Jina lako liwe Seba Bwiri, jina la mlezi/mzazi wako liwe George Bwiri Mahaba wa S.L.P 280 Musoma. Anuani yako iwe S.L.P 25458 Dar es salaam.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Uandishi wa anuani juu ya bahasha

Mwandishi wa barua amalizapo kuandika barua, huikunja na kuiingiza kwenye bahasha na kuipeleka posta tayari kwa kuituma kwa mlengwa. Mara nyingi juu ya bahasha ni lazima kuwekwe stempu ambayo ndio hubeba gharama ya kuisafirisha barua hiyo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Stempu hubandikwa juu ya bahasha upande wa kulia juu nchani mwa bahasha. Anuani inayoandikwa juu ya bahasha huwa na muundo maalumu kama ifuatavyo:

 

 

STEMPU

 

 

 

SEPHANIA KAZUMBA,

   S.L.P   23,

      BUKENE – NZEGA.

 
                                                                                                         

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 


              

 

Zoezi la Mada

1.  Chagua herufi ya jibu sahihi katika vipengele (i) hadi (v) kisha andika herufi ya jibu hilo katika sehemu ya kujibia.

i)            Ni sehemu gani katika muundo wa insha za wasifu huonesha mapendekezo ya mwandishi kuhusiana na jambo linalojadiliwa?

A.  Kichwa cha insha

B.  Hitimisho

C.  Kiini cha insha

D. Utangulizi

E.  Hoja za insha

 

ii)          Ipi ni hatua ya mwisho ya kuzingatia katika kuandika ufupisho wa habari uliyosoma?

A.  Kuhesabu idadi ya maneno

B.  Kutambua mawazo makuu

C.  Kusoma kwa makini

D. Kuandika idadi ya maneno

E.  Kuandika kichwa cha habari

 

iii)        Ipi ni alama ya uandishi inayotumika kuonesha sehemu mbili za sentensi zilizo kinyume?

A.  Nukta pacha

B.  Mkato

C.  Nukta mbili

D. Nukta mkato

E.  Nukta mtajo

 

 

 

iv)         Nitawaadhibu wote”, Mwalimu Gudilla  alisema. Ni alama ipi ya uandishi imetumika katika sentensi nitawaadhibu wote?

A.  Alama ya mshangao

B.  Alama ya ritifaa

C.  Alama ya mtajo

D. Alama ya mjalizo

E.  Alama ya kushangaa

 

v)           Lipi kati ya maneno yafuatayo huandikwa mwanzoni mwa barua ya kirafiki?

A.  Saini ya mwandishi

B.  Dada yangu mpendwa

C.  Tarehe

D. Anwani ya mwandishi

E.  Jina la mwandishi

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

2.  Oanisha maana za dhana za alama za uandishi zilizo katika Safu A kwa kuchagua herufi ya dhana husika katika Safu B kasha andika herufi husika katika sehemu ya kujibia.

 

 

 

 

Safu A

Safu B

i)            Huonesha vipimo mbalimbali katika desimali

ii)          Hutumika ili kupumzika katika sentensi iliyo ndefu sana

iii)        Huonesha uwiano baina ya namba

iv)         Hutumika badala ya nukta mbili

v)           Huonesha maana ya ziada katika sentensi

A.  (:)

B.  (-)

C.  (;)

D. (.)

E.  ( )

F.  (?)

G. (!)

 

 

 

3.  Panga vipengele vifuatavyo kwa kufuata muundo wa barua ya kirafiki.

i)          Salamu za awali

ii)        Tarehe

iii)      Furaha Amani

iv)       Shule ya Sekondari Kifungilo, S.L.P 248 Tanga

v)         Barua yenyewe

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

4.  Andika maneno matano (5) kutokana na jedwali lifuatalo na ueleze umuhimu wa maneno hayo kama yanavyoweza kutumika katika barua ya kirafiki.

A

 

M

W

A

N

Z

O

W

A

B

M

 

N

A

M

A

E

E

A

U

A

A

 

U

U

L

A

S

A

S

Y

R

T

 

L

A

A

S

P

T

L

N

U

A

 

K

J

I

N

A

B

P

N

A

N

 

Z

A

I

E

I

B

E

D

E

O

 

O

K

L

N

E

T

I

O

A

T

 

A

R

E

H

E

E

I

N

A

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

5.  Tumia vipengele vilivyomo kwenye kisanduku kujaza muundo wa barua ya kirafiki uliyopewa.

Anwani ya mwandishi, Jina la mwandishi, Tarehe ya kuandika barua, Mwanzo wa barua, Mwisho wa barua, Barua yenyewe

 
 

 

 

 


 

 
                             

 

 

 

 

 

 
 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 


6.  Tia alama za uandishi zifaazo kusahihisha sentensi zifuatazo.

(a) Wanafunzi walisema kwa pamoja tutashinda

(b)Daudi alikuwa kibaraka cha wazungu

(c) Rebeka George Kyamba aliwaeleza wanafunzi wamesema tutasoma kwa bidii

(d)Endelea twasikiliza hivyo basi Meneja aliendelea.

 

7.  Andika insha yenye maneno yasiyopungua mia mbili (200) na yasiyozidi mia mbili na hamsini (250) juu ya mada moja kati ya zifuatazo.

(a) Ajali za barabarani

(b)Nilipomaliza darasa la saba

(c) Umuhimu wa kujisomea

(d)Madhara ya ajira kwa watoto

(e) Unyanyasaji wa kijinsia.

 

8.  Badilisha kadi ya mwaliko ifuatayo iwe barua ya kirafiki.

 

MWALIKO WA HARUSI

Familia ya Mzee Charles Swai wa Dar es salaam,            wanayo furaha kubwa sana kukualika/kuwaalika

Prof/Dkt/Shekhe/Padri/Bw/Bi

Bi Asha Kizuki

Kwenye harusi ya kijana wao mpendwa Godson Swai

Itakayofanyika katika Ukumbi wa diamond jubilee siku ya Jumamosi tarehe 6/8/2022 kuanzia saa moja jioni.

Kufika kwako ndiyo mafanikio ya shughuli hii

Majibu ( kwa wasiofika tu)

Gloria Swai.

Simu na. 0684 224 944

 

 

 
 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 


9.  Fafanua mambo matano ya kuzingatia unapoandika insha ya wasifu.

 

10. Chunguza picha ifuatayo kisha tunga insha isiyopungua maneno mia moja.

 

 

 

 

Picha ya vijana wakitumia sindano za dawa za kulevya

 
 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

0 maoni:

Post a Comment

Powered by Blogger.

Wasiliana nami papo kwa papo

Name

Email *

Message *

Ads 468x60px

Breaking News

Top Featured

Featured Posts

Sample text

Sample Text

Recomended

Facebook

Advertise

Most Popular

Connect With Us

Followers

Social Icons

Pages

Pages

BTricks

Pages

Popular posts

Tafuta chochote ukiwa hapahapa

Kategori

Recent Comments

You can replace this text by going to "Layout" and then "Page Elements" section. Edit " About "

recent posts

Video Of Day

TRANSLATE

Instructions

Video

Flickr Images

FURAHIA UWEPO WAKO HAPA

Logo Design by FlamingText.com
Logo Design by FlamingText.com

Imetembelewa mara

NUMBER OF VIEWERS

Popular Posts

SAJIRI

Definition List

premium-wordpress-themes.org