Kuwasiliana kwa njia ya mazungumzo
Dhana
ya Mazungumzo.
Mazungumzo ni utaratibu wa kuongea
baina ya pande mbili ambapo wahusika wa mazungumzo hayo huwa ni watu. Kwa
kawaida mazungumzo huwasilishwa kwa njia ya mdomo na huweza kuambatana na ishara
za viungo vya mwili. Chanzo cha mazungumzo huwa ni mzungumzaji na kikomo chake
huwa ni msikilizaji.
Mzungumzaji
huwa ni mtu anayeanzisha uneni, huyu kifasihi huitwa fanani. Uneni ni utoaji wa
matamko yenye maana katika lugha fulani ilihali kitendo ni dhana ya utendaji .
Msikilizaji huwa ni mtu anayepokea uneni kutoka kwa mzungumzaji huyu kifasihi
huitwa hadhira.
Misingi ya Mazungumzo
Ili watu
waweze kuelewana vizuri wanapozungumza ni lazima wazingatie mambo makuu
yafuatayo,Pia mambo hayo yasipozingatiwa yanaweza kuathiri mazungumzo ya
wazungumzaj
(i)
Uhusiano wa wazungumzaji
Unaweza
kuelewa na kutambua uhusiano wa watu wanaozungumza kama ni marafiki , wapenzi,
baba na mtoto au mwalimu na mwanafunzi watu au wazungumzaji ni maadui kwa
kuangalia msamiati wanayotumia katika mazungumzo yao. Msamiati wanayotumia
katika mazungumzo yao. Msamiati anayotumia mwalimu na mwanafunzi wake ni
tofauti sana na msamiati anayotumia mtoto na wazazi wake kwa sababu , msamiati
utakaotumika na mwalimu na mwanafunzi
wake hutawaliwa na heshima busara na ulezi zaidi tofauti na msamiati
utakaotumika na mtoto na wazazi wake kwani yenyewe hatawaliwa na madoido,
madokezo na mabembelezo zaidi.
(ii)
Mada inayozungumzwa
Mazungumzo
hutawaliwa na mada , mazunguzumo huhusisha mada inayozungumzwa ambayo pia
huamua msamiati kwa kutumia katika mazungumzo husika. Kwa mfano mada inaweza
kuwa siasa, masomo, sherehe au muziki. Wazungumziaji wana takiwa kuchagua
msamiati kulingana na mada. Kwa mfano mada ya masomo inaweza kuibua msamiati
kama vile elimu, itifaki.
(iii) Muktadha wa Mazungumzo
Mazungumzo
huathiriwa na miktadha tofauti tofauti muktadha wa mazungumzo unaweza kuwa
rasmi au usiwe rasmi, kuna miktadha mbalimbali ambayo wazungumziaji huweza
kutumia wakati wa mazungumzo yao. Miktadha kama hiyo ni shuleni, dukani, mjini,
barabarani, kijijini n.k . Kwa mfano , lugha anayotumia daktari hospitalini ni
tofauti na lugha anayotumia daktari huyohuyo akiwa nyumbani kwake hivyo lugha
hutofautisha kulingana na muktadha wazungumzaji wanapaswa kuzingatia muktadha
wa mazungumzo yao.
Mfano.
Mazungumzo ya mama na mwanae wakiwa
kwenye daladala.
MTOTO:Mama , mbona kila siku baba anakupiga?
MAMA:Chukua andazi mwanangu.
Kwa mfano
huu, Mama amezingatia muktadha ndio maana hahitaji mazungumzo yaendelee , kwani
mada husika haifai kuzungumziwa kwenye daladala
(iv)
Lengo la mazungumzo
Mzungumzaji
huwa na lengo la kuzungumza anapokutana na mwenzake ili kukidhi lengo la
mazungumzo, mzungumzaji huhitaji kutoa ufafanuzi wa yale anayoyasema ili
msikilizaji aelewe kama ilivyokusudiwa . Lengo la mazungumzo linaweza kuwa
kutoa taarifa , kuhoji, kukejeli ,kuelimisha ,kuonya au kutia moyo.
(v)
Muda /wakati wa mazungumzo
Mzungumzaji
ni lazima ateue msamiati utakaoendana na wakati katika eneo husika . Matumizi
mabaya ya muda katika eneo amabalo si rafiki hufanya mazungumzo kuchosha.
(vi)
Utanzu au aina ya mawasiliano
Kabla ya
mazungumzo , mzungumziaji ni lazima ajiulize kwamba ujumbe aliokusudia
kufikisha kwa hadhira ataufikisha kwa mbinu ipi? Mbinu ya majadiliano,
masimulizi, hotuba au nyimbo.
(vii) Shughuli inayofanyika
Msamiati
unaotumika katika mazungumzo huendana na shughuli inayohusika kwa mfano kama
shughuli inayofanyika ni ufugaji , uchimbaji madini na msamiati wake utaendana
na shughuli husika.
Mifano ifuatayo inaonesha mazungumzo
katika miktadha tofauti.
Mfano
1 Mazungumzo ya kanisani
MCHUNGAJI: Bwana Yesu apewe sifa
WAUMINI: Amina
MCHUNGAJI: Naomba mfungue biblia zenu.
Mfano
2 Mazungumzo ya marafiki.
BAHATI: Mambo sanura?
SANURA: Poa tu vipi wewe?
BAHATI :Fresh rafiki yangu, vipi jana mama hakukutia ndimu
ulipochelewa kurudi?
SANURA: Loo! Mama Yule na ule mdomo wake, alinichimba biti sana.
Mfano
3. Mazungumzo ya shuleni
MWANAFUNZI:Shikamoo mwalimu
MWALIMU: Marahaba , hujambo?
MWANAFUNZI: Sijambo
(viii) Hali za wahusika wakati wa mazungumzo
Lugha
inayotumika inapaswa kuendana na hali za wahusika wakati wa mazungumzo ili
kuleta maelewano . kwa mfano kama mzungumzaji ni mgonjwa au amekasirika, lugha
inayotumika kuwasiliana naye itaendana na hali hiyo.
Andaa
mazungumzo yanayoweza kuzungumzwa katika maeneo yafuatayo; a) Hospitalini b) stendi ya mabasi c) Dukani d) Sokoni e) Shuleni
ZOEZI
Hatua za kufanya mazungumzo katika
lugha ya kiswahiliKatika
kufanya mazungumzo zipo hatua mbalimbali za kufuata wazungumzaji wanapokutana
kuzungumza , Hatua hizo ni hizi zifuatazo;
Salamu
Watu
wawili wanapokutana kuzungumza sharti wasalimiane kabla ya kuanza mazungumzo
hayo, Jambo la kwanza huwa ni salamu, salamu hii huwa rasmi au isiyo rasmi
kutegemea na uhusiano uliopo baina ya wazungumzaji , Salamu rasmi inaweza kuwa
kama ifuatavyo; Habari za asubuhi na habari za kazi, Salamu zisizo rasmi
inaweza kuwa hujambo? Mambo, vipi hali yako, kumbuka kuwa “kwa heri “ siyo
salamu.
Utambulisho
Wazungumzaji
wanapokutana wana nafasi ya kutambuana . kipengele hiki hufanyika mara baada ya
wahusika kusalimiana katika utambulisho wazungumzaji hutaja majina yao na
wasifu wao kwa ujumla. Kwa mfano, unaitwa nani, wewe ni nani?. Hii huwasaidia
wazungumzaji kujenga mipaka, uhusiano na mazoea , ukimtambua mtu unayezungumza
naye itakupa urahisi wa kuchagua msamiati utakaotumia unapozungumza naye.
Mazungumzo
mafupi
Mara
baada ya utambulisho , wazungumzaji hufanya mazungumzo mafupi kwa nia ya kutaka
dhima ya mazungumzo yao.
Mazungumzo
kamili
Mazungumzo
kamili hutegemea muktadha, lengo la mazungumzo , mada ya mazungmzo na uhusiano
uliopo baina ya wazungumzaji . Ni sehemu hii ambayo hutumia muda mrefu wakati
wa mazungumzo.
Ufafanuzi
Ni
kipengele kinachohusu mambo yote ambayo hayakueleweka kwa mmoja kati ya
wazungumzaji ,hivyo kurudiwa na kutolewa maelezo ya ziada.
Kukatisha
Mazungumzo
Kipengele
hiki ni muhimu sana wakati wa mazungumzo, mathalani umetembelewa na ndugu yako
ofisini kwako, kwa bahati mbaya ndugu yako huyo anaongea sana kiasi kwamba
wageni wengine wanalalamika nje ya ofisi inakupasa ukatishe mazungumzo . zipo
njia mbalimbali za kukatisha mazungumzo mfano, kama umekaa kwenye kiti unaweza
kusimama kisha kumsogelea na kumpa mkono mtu unayezungumza naye ukaongea naye
kwa maneno kama vile “Nitakushukuru, karibu tena, tuonane wakati mwingine n.k
Kuagana
Tumia
maneno kulingana na muktadha mfano kama ni ofisini waweza kutumia maneno rasmi
kama vile “Nakutakia kazi njema, kila la kheri , tuonane wakati mwingine na
unaweza kutumia maneno kama vile baadaye furahia siku yako katika muktadha usio
rasmi.
Lugha
fasaha
Lugha fasaha ni ile ambayo inafuata
taratibu zote za lugha hiyo ikizingatia maana, matamshi, muundo na mantiki.
Lugha inapotumika vibaya huweza kupotosha lengo la mzungumzaji. Makosa haya
yanaweza kujitokeza katika msamiati (maana) miundo, matamshi na mantiki. Kwa
mfano, Kurara, neno hili si neno fasaha kwa sababu katika lugha ya Kiswahili
hutamkwa kulala. Ili mazungumzo yaweze kuwa mazuri, wazungumzaji lazima watumie
lugha kwa ufasaha. Angalia makosa mbalimbali ambayo huweza kufanywa na
watumiaji wa lugha fasaha katika misingi ya maana, miundo, matamshi, kuacha
baadhi ya maneno, kuongeza vitamkwa au silabi, makosa katika matumizi ya
nyakati na mantiki.
(i)
Makosa ya kimaana / Kimsamiati
Ili lugha iwe fasaha ni sharti neno
lililokusudiwa liwe fasaha. Kuna maneno mengi yenye maana zaidi ya moja. Maneno
haya ni kama vile, kaa, kata, chungu, mbuzi, kanga, barabara, panda, susa,
kanda.
Tazama namna maneno haya yanavyoweza
kuleta dhana nyingine:
§ Susa -
Tikisa mti
-
Uchafu utokanao
na mabaki ya chakula
-
Kataa kufanya
jambo
-
Sehemu ya muwa
isiyo tamu
§ Kata -
Eneo la kijiografia
-
Gawanyisha kitu
katika vipande
- Chezesha
viungo vya mwili kama vile macho,kiuno shingo.
Hapa
ndipo maneno kuwakilisha badala ya kuwasilisha, baada badala ya badala
hufafanuliwa.
Mfano
l
Mvu imepiga sana usiku badala ya mvua imenyesha sana usiku
l
Mwalimu alidondoka mlangoni badala ya mwalimu alianguka
mlangoni
l
Spika alimwasilisha Rais badala ya spika
alimwakilisha Rais
l
Ashura amenona sana badala ya Ashura amenenepa
sana
l Ng’ombe amejifungua badala ya
ng’ombe amezaa
Baadhi ya
maneno ambayo tofauti zake za kimaana zinatofautishwa na mkazo katika jinsi
neno linavyotamkwa.
(ii)
Makosa ya kimuundo
Mpangilio mzuri wa maneno katika sentensi
hufanya lugha kuwa fasaha. Mfuatano wa maneno husaidia kuleta maana
iliyokusudiwa. Kwa mfano “Wanaitwa wanafunzi badala ya Wanafunzi wanaitwa”.
“Kizinga anaitwa na Juma” badala ya Kizinga na Juma wanaitwa.
(iii) Makosa ya kimatamshi
Matamshi
mazuri ya sauti za lugha hujenga ufasaha wa lugha hiyo. Watu wengine hushindwa
kutamka baadhi ya sauti za Kiswahili kwa sababu ya athari za lugha mama na
athari za kimaumbile, hususani kithembe, kibogoyo na toinyo. wengine
huchanganya na kubadili sauti hizo. Mifano ya maneno haya ni kama yafuatayo:
Ngombe badala ya ng’ombe
Mbusi badala ya mbuzi
Kurara badala ya kulala
Zambi badala ya dhambi
Langi badala ya rangi
Zarura badala ya dharura
Ntu badala ya mtu
Thatha badala ya sasa.
(iv)Makosa ya kimuundo
Haya ni makosa ambayo hutokana na
kutokuwa na mpangilio mzuri wa maneno katika sentensi.Mara nyingi sentensi za
Kiswahili kimuundo huanza na nomino au kiwakilishi,kisha hufuatiwa na
kivumishi,hufuata kitenzi na kisha aina nyingine za maneno.Baadhi ya
wazungumzaji hushindwa kufuata utaratibu huu na kujikuta wakikosea kama mifano
ifuatavyo inavyoonekana;Kiti mimi nina badala ya mimi nina kiti.
Mama chakula anapika badala ya Mama
anapika chakula
(v)Makosa ya kuongeza vitamkwa.
Ni makosa ambayo hufanywa na
watumiaji wa lugha kwa
kuongeza vitamkwa au silabi katika
maneno sehemu
ambapo hapatakiwi.Mara nyingi makosa
kama haya
husababishwa na athari za lugha
mama.
Mfano;
Msichana msafi anaitwa
badala ya msichana safi anaitwa.
Mimi nakuambiaga badala ya
mimi huwa nakuambia.
Mashuleni pawe safi badala
ya shuleni pawe safi.
(vi)Makosa ya kuacha maneno
Ni makosa ambayo watumiaji wa lugha huacha kuyatamka au kuyatumia baadhi
ya maneno fulani katika sentensi wakiamini kuwa ujumbe walioukusudia utakuwa
umefika kwa hadhira.
Mfano,
Baba amerudi kazini badala ya baba amerudi kutoka kazini.
(vii)Makosa ya Mantiki
Ni utaratibu mzuri wa kufikiri ili
kupata maana iliyolengwa. Kwa mfano:
-
Mfupa hauna ulimi badala ya ulimi hauna mfupa.
-
Chai imeingia nzi badala ya nzi ameingia kwenye chai.
-
Nimemkuta hayupo badala ya sijamkuta.
-
Kitumbua kimeingia mchanga badala ya mchanga umeingia
ndani ya kitumbua.
Umuhimu
wa kutumia lugha kwa ufasaha
·
Hufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa urahisi zaidi.
·
Huifanya lugha kuwa na thamani na hadhi kubwa.
·
Huwavutia watu na kuwafanya kujifunza lugha kirahisi.
·
Huifanya lugha ikubalike ndani na nje ya nchi.
·
Huboresha uhusiano wa watumiaji wa lugha husika.
·
Hufanya lugha iwe na mvuto na yenye kushawishi watumiaji
wapya.
·
Hudumisha sarufi ya lugha.
·
Hukuza na kuendeleza utamaduni wa jamii.
Athari za kutotumia lugha kwa ufasaha
(i)
Kupata maana ambayo haijakusudiwa.
(ii)
Watumiaji kutoelewana.
(iii)
Lugha kushuka hadhi yake na kuonekana kama ni lugha ya
wahuni.
(iv)
Inaweza kuchochea ugomvi baina ya watumiaji kutokana na
kutoelewana hasa wakati wa utumiaji wa msamiati.
(v)
Kuondoa umoja na mshikamano kwa sababu tu lugha ndio
kiunganishi cha watu hasa wanaoelewana.
(vi)Hudumaza utamaduni wa jamii.
(vii)Husababisha ujumbe ushindwe kufika
kama ulivyokusudiwa.
Zoezi la mada
1.
Chagua herufi ya jibu sahihi katika vipengele (i) – (v),
kisha andika herufi ya jibu hilo katika sehemu ya kujibia.
(i)
Mawasiliano baina ya wanyama, ndege na wadudu hayawezi
kuitwa lugha kwa sababu gani?
A.
Vitamkwa vyao ni hafifu
B.
Lugha ni mali ya wanyama tu
C.
Vitamkwa vyao havina maana
D. Vitamkwa vyao havina irabu
E.
Vitamkwa vyao ni vya msingi katika utamkaji
(ii)
Kanuni maalumu na taratibu za lugha zinazofuatwa na
wazungumzaji katika mawasiliano huitwaje?
A.
Lugha B.
Sarufi C. Lugha fasaha D. Utumizi wa lugha E. Mawasiliano
(iii)
Neno abab
halikubaliki lakini neno baba
linakubalika kwa sababu gani?
A.
Mpangilio wa neno
B.
Mpangilio wa irabu
C.
Mpangilio wa vitamkwa
D. Mpangilio wa fonimu
E.
Mpangilio wa mofimu
(iv)
Dhima kuu ya lugha katika mawasiliano ni ipi kati ya hizi
zifuatazo?
A.
Kutambulisha utamaduni
B.
Kutunza historia
C.
Kupashana habari
D. Kuelimisha jamii
E.
Kuburudisha jamii
(v)
Zipi ni aina mbili za fonimu katika lugha ya Kiswahili?
A.
Irabu na konsonanti
B.
Irabu na silabi
C.
Irabu na mofimu
D. Konsonanti na kiambishi
E.
Foni na alofoni
2.
Oanisha dhana zilizopo safu A na mifano yake iliyopo safu
B kwa kujaza herufi ya jibu sahihi kwenye safu A.
Safu A |
Safu B |
(i)
Vokali
(ii)
Haitamkiki
bila kuwekewa irabu (iii)
Huundwa
kwa sauti ya konsonanti (iv)
Huundwa
na irabu pamoja na konsonanti (v)
Huunda
lugha |
A. Sauti B. Neno C. Silabi D. Konsonanti E. Lugha F. Mfumo G. Nasibu |
3.
Panga fonimu hizi kwa utaratibu unaofaa ili kujenga neno
la Kiswahili.
(a) Ambit
(b) Awsa
(c) Ynmzaa
(d) Orsdai
(e) ngzoao
4.
Eleza kwa kifupi dhima kuu tano za lugha
5.
(a) Fafanua
maana ya lugha fasaha
(b) Fafanua madhara matano (5) ya kutumia
lugha isiyo fasaha
6.
Eleza tofauti baina ya sauti hizi
(a) /a/ na /p/
(b) /g/ na /t/
(c) /f/ na /ng/
(d) /th/ na /n/
(e) /w/ na /y/
7.
Eleza maana ya dhana zifuatazo
(i)
Lugha
(ii)
Lugha fasaha
(iii)
Irabu
(iv)
Konsonanti
(v)
Silabi
8.
Sahihisha sentensi zifuatazo
(a) Doto ameungama zambi zake
(b) Watoto walirara sakafuni
(c) Mzee Kapinga anapaka langi nyumba
yote
(d) Masanja amewasili jana kutoka ngambo
(e) Mbusi hii inapenda kutoroka sana.
9.
Eleza maana mbili za kila neno
(a) Paa
(b) Vua
(c) Panda
(d) Randa
(e) Kanda
10. Fafanua mambo ya kuzingatiwa ili
kuwezesha mawasiliano katika mazungumzo.
0 maoni:
Post a Comment