Imeandaliwa na Mtila Mswahili
Nadharia ya
uchanganuzi vijenzi maana ni mtazamo muhimu katika semantiki. Nadharia hii, iliyoasisiwa na kutumiwa na wanaanthropolojia wa Kimarekani,
inachunguza maana ya maneno kwa kuyagawa katika vijenzi vidogo vya maana.
Mtazamo huu ulitumika hasa kueleza maneno ya ukoo. Iliaminika kuwa maneno
yalijengwa kwa vijenzi fulani ambavyo vinaweza kubainishwa na kwa hiyo kuelezea
neno hilo.
Kila neno linaeleweka kupitia seti ya sifa
bainifu zinazoliweka katika kategoria yake. Vijenzi hivi husaidia kueleza
uhusiano kati ya maneno, kama vile usinonimia, antonimia, na hiponimia. Kwa
mfano tutazame mifano ifuatayo:
"Mwanaume" inaweza kuchanganuliwa
kuwa na vijenzi kama [+binadamu], [+hai], [+mume], na [+mtu mzima].
"Mwanamke" itakuwa na vijenzi kama
[+binadamu], [+hai], [+mke], na [+mtu mzima].
"Mtoto" itakuwa na vijenzi kama
[+binadamu], [+hai], na [-mtu mzima].
Hivi ndivyo
vijenzi vinavyoeleza maana za maneno haya . Kwa mujibu wa wana nadharia
ambao hutumia mtazamo huu, vijenzi hivi ndivyo vinavyojenga maana ya
kijumla ya maneno hayo.
Na rangi ni
ule muonekano ambao huwepo katika kitu, muonekano huo huashiria maana fulani.
Maana hizo zinaweza kuwa ni za kifalsafa, kimsingi na kiutamaduni. Rangi
inaweza kutofautiana kutokana na muktadha unaotumika. Kwa mfano katika uongozi rangi nyeusi
humaanisha nguvu, lakini pia katika mazishi rangi nyeusi humaanisha kifo au
huzuni.
Katika lugha
ya Kiswahili Kuna rangi kuu tatu, ambazo ni nyeusi, nyekundu, na nyeupe. Na rangi nyengine
zimetokana na rangi hizo. Kwa mfano rangi ya zambarau na rangi ya kijani.
Dhana ya
rangi huwa na sifa nyingi ambazo hubainisha kazi mbali mbali. Sifa zenyewe ni
hizi zifuatazo:
[+rangi]
[+dhahania]
[+ rangi yenyewe]
[- sio rangi yenyewe]
Kwa hivyo, kwa kutumia nadharia ya
uchanganuzi vijenzi maana, nitaonyesha sifa bainifu za maana ya rangi tatu katika lugha ya Kiswahili kama ifuatavyo:-
Rangi Nyekundu
Rangi hii huweza kuchanganuliwa kuwa na
vijenzi Maana kama:
[+damu]
[+moto]
[+upendo]
[+hatari]
[+nguvu]
[-Tulivu]
Sifa bainifu
ya rangi hii ni kuwa, rangi nyekundu ni
rangi ambayo huonesha ishara ya upendo katika ulimwengu. Kwa mfano katika jamii
hii ya Waafrika, mara nyingi hutumika katika harusi au siku ya Wapendanao (
Valentine day). Aidha rangi hii huonesha ushindi, hatari, shauku, damu, na
uchungu. Katika utamaduni huashiria sherehe za ndoa na furaha. Na katika
falsafa rangi nyekundu huashiria nguvu ya maisha na shauku ya kibinaadamu.
Rangi
Nyeusi
Rangi hii huchanganuliwa kuwa na vijenzi Maana
kama:
[+huzuni]
[+giza]
[+siri]
[+ukosefu wa nuru]
[+kifahari]
[-Uangalifu]
[-Amani]
Sifa bainifu
ya rangi nyeusi, ni rangi ambayo baadhi ya wanajamii wanaamini kua ni rangi
ambayo huonesha ishara ya kitu, kifo, msiba, giza, majuto, nguvu, huakisi
ukosefu wa nuru, huweza kuwakilisha mambo ya kifahari, ukuu na heshima. Rangi hii huwasilisha rangi ya Waafrika ambao
ni weusi. Vile vile huonesha ishara ya
uchawi wanapovaa nguo kwa ajili ya kufanya kazi zao za kishirikina. Na katika
falsafa, rangi nyeusi huashiria ulimwengu wa siri na mambo yasiyojulikana.
Rangi nyeupe
Rangi hii
itakuwa na vijenzi Maana kama:
[+amani ]
[+usafi]
[+utakatifu]
[+Mwanga]
[+Uangalifu]
[-Giza]
Sifa Bainifu ya rangi hii ni kuwa, rangi nyeupe huweza kuashiria amani,
mwanga, uangalifu, usafi, na utakatifu. Pia rangi hii inaweza kuashiria kifo,
huzuni, na roho. Vile vile katika
tamaduni za uswahilini rangi nyeupe hutumika katika mazishi na huashiria kifo
na huzuni. Na katika falsafa huashiria
ukamilifu wa kiroho na utukufu.
Kwa ujumla, Uchanganuzi wa vijenzi maana husaidia
kuonyesha sifa bainifu za maana ya neno. Hivyo basi, kwa upande wa rangi
tunatakiwa tufahamu kuwa, maana ya rangi inaweza kutofautiana kulingana na
muktadha na tamaduni. Kwa hivyo ni muhimu kuzingatia muktadha unaotumika wakati
wa kufasiri maana ya rangi katika lugha ya Kiswahili. Kwa mfano rangi huweza kutumika katika kueleza hisia za
kibinaadamu, mfano hisia za huzuni, hisia
za furaha, hisia za upendo na kutisha. Hata hivyo, rangi huwa ni ishara ya
kiimani, kwa mfano Waganga wa kienyeji hutumia rangi kama vile nyekundu, nyeupe na nyeusi humaanisha dhana ya kishetani.
MAREJEO:
Habwe, J
& Karanja, P. (2004). Misingi ya sarufi ya Kiswahili. Nairobi : Phoenix Publishers Ltd.
Chomsky, N. (1965). Aspects of the Theory of
Syntax. MIT Press.
Katz, J. J., & Fodor, J. A. (1963). The
structure of a semantic theory. Language, 39(2), 170-210.
Lyons, J. (1977). Semantics (Vol. 1).
Cambridge University Press.
Leech, G. N. (1981). Semantics: The study of
meaning. Penguin Books.
Cruse, D. A. (1986). Lexical semantics.
Cambridge University Press.
Allan, K. (2001). Natural language semantics.
Blackwell Publishing.
Nida, E. A. (1975). Componential analysis of
meaning: An introduction to semantic structures. Mouton.
0 maoni:
Post a Comment