Imeandaliwa na Mtila Mswahili.
UTANGULIZI
Kwa
mujibu wa Omolewa (2007) elimu ya jadi ni mchakato endelevu wa mafunzo kupitia
maisha ya kila siku, ambapo jamii inawajibika kumfundisha mtoto maadili, ujuzi
na mila kwa lengo la kumwezesha kuishi kwa mafanikio ndani ya jamii yake.
Pia
Wane (2021) anafafanua kuwa thieta za kijadi ni sanaa ya mawasiliano ambayo
huunganisha maonyesho ya uigizaji, nyimbo, ngoma, na mazungumzo kama njia ya
kujifunza na kuendeleza maarifa ya jamii.
Aidha,
Chikoko (2022) anafafanua thieta za kijadi kama njia ya kuelezea matukio au
masuala ya kijamii kwa kutumia vipengele vya sanaa ya utendaji kama sehemu ya
elimu isiyo rasmi kwa wanajamii.
Kwa
ujumla, thieta za kijadi ni aina ya elimu isiyo rasmi iliyotolewa kwa njia ya
vitendo, mazungumzo, maonyesho, na kushiriki katika shughuli za kijamii, ambayo
ililenga uendelezaji wa jamii kupitia maadili, ujuzi, na maarifa. Thieta za kijadi ni mfumo wa elimu
usio wa kiformali uliokuwepo katika jamii za Kiafrika kabla ya kuanzishwa kwa
shule rasmi na mfumo wa elimu ya Magharibi uliokuja na ukoloni. Thieta hizi
zililenga kuandaa mtu kuwa mshiriki mzuri wa jamii, mwenye maadili, ujuzi, na
maarifa ya kijamii.
Kabla
ya ujio wa ukoloni, jamii nyingi za Kiafrika zilikuwa na utamaduni tajiri wa
sanaa za maonyesho, ikiwemo sanaa ya thieta za kijadi. Thieta hizi zilihusisha
maonesho ya jukwaani yaliyofanyika katika mazingira ya asili au mikusanyiko ya
kijamii kwa lengo la kuelimisha, kuburudisha, kukuza maadili na kuendeleza
urithi wa jamii.
Thieta za kijadi hazikuhusiana tu na burudani bali pia
zilikuwa njia muhimu ya mawasiliano, mafunzo na utatuzi wa migogoro. Katika
jamii ya Kiafrika, thieta haikuhitaji jukwaa rasmi wala tamthilia
zilizoandikwa; bali ilitumia uigizaji wa moja kwa moja, nyimbo, ngoma, methali,
hadithi na maigizo ya maisha halisi. Zifuatazo ni badhi ya thieta za kijadi
zilizokuwa zikifanyika kabla ya ukoloni: -
Sherehe za maisha: Thieta hizi zilitolewa kupitia sherehe
za kijadi kama vile tohara, ubalehe, ndoa, na mazishi, ambazo zilifundisha
vijana kuhusu majukumu yao ya kijinsia, maadili, nidhamu, na utamaduni wa jamii
yao. Mfano, kwa jamii ya Wamakonde, wavulana walipitishwa kwenye
tohara (likumbi) ambako walijifunza kuhusu uongozi wa familia, heshima kwa
wazee, na namna ya kuwa wanaume wa kweli. Wakati wa tohara, walikaa kambini kwa
siku kadhaa wakipewa mafunzo ya maisha, kazi, na tabia njema. Kwa Wasambaa,
wasichana waliandaliwa kwa maisha ya ndoa kwa kufundishwa namna ya kutunza
familia, kupika, na kusimamia kaya. Sherehe hizi hazikuwa tu ibada bali
zilikuwa shule za maadili, uongozi, na utambulisho wa kijamii.
Simulizi
na hadithi: Hii ilikuwa mojawapo ya theita
mashuhuri ambapo wazee walitumia hadithi kufundisha watoto kuhusu maadili,
hila, haki, na hekima. Hadithi hizi mara nyingi zilihusisha wanyama kama
wahusika. Mfano, hadithi za Sungura na Fisi zilifundisha kuhusu
ujanja na matokeo ya tamaa. Sungura aliye mjanja huwakwepa maadui zake kwa
kutumia akili badala ya nguvu. Watoto
walijifunza kuwa wajanja na wasioonea wengine.
Hadithi hizi zilisimuliwa jioni na zilifuatana na maswali kwa watoto ili
kuthibitisha walichojifunza. Kwa hiyo, simulizi zilijenga uelewa wa
kijamii, mawasiliano, na maarifa ya maisha.
Nyimbo na mashairi ya kijadi: Nyimbo zilikuwa chombo cha kufundisha
maadili, historia ya jamii, na kazi mbalimbali za kijamii. Mashairi yalitumika
kueleza hali za maisha, kutoa nasaha, na kusherehekea matukio muhimu. Mfano,
kwa Wazaramo, nyimbo za mavuno kama “Lolea lolea twavuna mpunga” zilifundisha
mshikamano wa jamii, kazi ya pamoja, na umuhimu wa ardhi. Katika nyimbo za
harusi, wasichana walifundishwa kuhusu wajibu wao katika ndoa kupitia mashairi
yenye mafundisho kama vile: "Usipoamka mapema, chakula kitachomwa, mume
atakukasirikia, ndoa itavunjika.” Nyimbo hizo zilikuwa darasa la
wazi lenye mchanganyiko wa burudani na mafunzo.
Kazi za kijamii na mafunzo kwa
vitendo: Elimu ya jadi
ilitolewa kupitia kazi za kila siku ambapo watoto walijifunza kutoka kwa wazazi
na jamii kwa kushiriki moja kwa moja. Mfano ni mtoto wa Wanyakyusa
alijifunza kulima kwa kushiriki katika shamba la familia. Alijifunza kupanda,
kuvuna, na kuhifadhi mazao. Msichana alifundishwa kupika, kusuka vikapu, na
kushona kupitia kushiriki na mama na bibi katika kazi hizo. Elimu hii ilijikita
katika vitendo, na ilikuwa ya moja kwa moja, ikiimarisha ujuzi wa maisha na
uzalishaji.
Michezo ya kiasili: Michezo ilitumika kufundisha nidhamu,
ushirikiano, kujiamini, na kuhimili changamoto. Michezo pia ilichangia
maendeleo ya akili na mwili. Mfano, Mchezo wa bao la kete
ulifundisha kupanga mikakati, kuhesabu, na subira. Pia, kombolela na michezo ya
mbio ziliwafundisha watoto kufanya kazi kwa timu, uvumilivu, na ujasiri. Michezo
ilichukuliwa kama fursa ya kujifunza kwa njia ya furaha na kushirikiana.
Baraza la wazee na maamuzi ya kijamii:
Baraza la wazee
lilikuwa chombo cha maamuzi lakini pia kilitumika kama shule ya elimu ya jamii,
hasa kwa vijana waliotakiwa kujifunza kuhusu sheria za kijadi, uongozi, na
namna ya kushughulikia migogoro. Mfano, kwa Wairaqw, vijana waliambiwa
wahudhurie vikao vya baraza ili kusikiliza mijadala na uamuzi wa wazee kuhusu
masuala ya ardhi, ndoa, au migogoro ya familia. Kupitia hayo, walijifunza
kusuluhisha kwa amani, kuheshimu mamlaka, na kutambua nafasi ya kila mtu katika
jamii.
Matambiko na imani za jadi: Elimu ya kijadi pia ilitolewa kupitia
matambiko yaliyofanyika kuomba mvua, kuondoa mikosi, au kusherehekea mavuno.
Hii iliwafundisha vijana kuhusu imani, mazingira, na heshima kwa waliokufa. Mfano,
kwa Wagogo, kabla ya mavuno walifanya tambiko kwa mizimu kuomba mvua, ambapo walifundishwa
kuhusu umuhimu wa mazingira na ardhi katika maisha ya jamii. Katika tambiko la
matanga, vijana walielekezwa kuhusu heshima kwa wazazi waliokufa na maana ya
mshikamano wa ukoo.
Hitimisho
Thieta za kijadi kabla ya ukoloni zilikuwa mfumo wa kina na mpana wa elimu
uliolenga kukuza maadili, ujuzi, na mshikamano wa kijamii. Kupitia
sherehe za maisha, hadithi, nyimbo, kazi za kijamii, michezo, baraza la wazee
na matambiko, jamii ziliweza kuwalea watoto kuwa watu wazima wenye maarifa,
staha, na uwezo wa kuchangia maendeleo ya jamii. Ingawa mfumo huu haukuwa rasmi
kama shule za leo, ulitoa msingi madhubuti wa maisha ya kijamii na kiutamaduni.
MAREJEO
Chikoko,
V. (2022). Mifumo ya maarifa ya asili na mchango wake katika elimu kwa
maendeleo
endelevu barani Afrika. Jarida la Utafiti
wa Kielimu Barani Afrika, 10(1), 1–10. https://doi.org/10.30918/AERJ.101.21.092.
Omolewa, M. (2007). Mbinu za jadi za
elimu barani Afrika: Umuhimu wake katika dunia
ya sasa. Mapitio ya Kimataifa ya
Elimu, 53(5-6), 593–612.
https://doi.org/10.1007/s11159-007-9060-1.
Wane, N. N. (2021). Maarifa
ya jadi ya Kiafrika na elimu: Upatanisho kati ya yaliyopita na
ya
sasa. Jarida la
Kimataifa la Utafiti wa Mwamko wa Kiafrika, 16(1), 34–50. https://doi.org/10.1080/18186874.2021.1902748.
0 maoni:
Post a Comment